………….
CHATO
KATIKA kuhakikisha jamii zilizoko pembezoni mwa makao makuu ya wilaya zinanufaika na huduma bora za afya, Serikali inakusudia kuipandisha hadhi zahanati ya Kasenga wilayani Chato mkoani Geita kuwa kituo cha afya hatua itakayosaidia kusogeza huduma za upasuaji karibu.
Hatua hiyo inatajwa kunusuru afya za wajawazito,watoto na wazee ambao wanalazimika kutembea umbari mrefu zaidi ya km 13 ili kufika kwenye kituo cha afya Kachwamba.
Kutokana na hali hiyo serikali imelazimika kuipatia zahanati hiyo kiasi cha milioni 250 kwaajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, kichomea taka, shimo la majivu, shimo la kutupia kondo la nyuma na uzio wa kuzunguka majengo yaliyopo.
Ili kuhakikisha ujenzi huo unazingatia viwango vilivyokusudiwa, Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, amelazimika kufanya ziara ya kikazi ili kujionea upanuzi huo kisha kuzungumza na wananchi wa kata hiyo.
Akiwa katika Kata hiyo, Bura amewapongeza viongozi wote walioshiriki katika usimamizi wa jengo hilo kutokana na kuridhishwa na ubora wake na kwamba ipo haja kwa serikali kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mingine ya umma.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo mbele ya mkuu wa wilaya, Mganga mkuu wa Zanahati hiyo, Michael Mathias, amesema utekelezaji wa upanuzi huo umetokana na kupokea fedha kutoka mpango wa uwekezaji katika Afya ya mama na mtoto( TMCHIP).
Hata hivyo amedai jamii ya Kasenga imeupokea mradi huo kwa furaha na kuamua kutoa ushirikiano mkubwa ikiwemo kusafisha eneo la mradi pamoja na jamii kushiriki katika uchimbaji wa msingi wa jengo la OPD.
Kadhalika zahanati hiyo imepokea kiasi kingine cha shilingi 239,748,571 kutoka serikalini kwaajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi na chumba upasuaji kwa pamoja(maternity complex).
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kasenga, Damian Nzilaliye, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutambua adha kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa kata hiyo kwa kutembea na kutumia gharama kubwa kufuata huduma za afya maeneo mengine.
Amesema kupandishwa hadhi kwa zahanati hiyo itasaidia jamii kupata huduma bora za afya na kwa ukaribu zaidi, hali itakayosaidia kupatikana kwa maendeleo ya haraka baada ya muda mwingi kuutumia katika uzalishaji mali
Mwisho.



