Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amewataka viongozi wa Serikali wakae na kujadiliana namna ya kuondoa mambo yanayokwaza utalii wa dini, ambao Tanzania ina fursa lukuki lakini hainufaiki nazo ipasavyo.
Hoja ya Zungu imetokana na kile alichofafanua kuwa Tanzania ina utajiri wa historia za kidini, ikiwemo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, kuwahi kuishi nchini, lakini hazitumiki kama fursa za utalii na kuiingizia nchi fedha.
Papa Leo aliingia nchini mwaka 2003 alipokuwa Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino Duniani.
Alipita katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Njombe na Ruvuma. Akiwa Songea mkoani Ruvuma, alitembelea nyumba ya malezi ya shirika hilo.
Zungu anakuja na hoja hiyo wakati ambapo soko la utalii wa dini linaendelea kuongezeka duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za Religious Tourism, inakadiriwa thamani ya soko la kimataifa la utalii wa kidini lilifikia takribani dola bilioni 254.3 (zaidi ya Sh655.1 trilioni) mwaka 2023.
Hata hivyo, thamani hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia karibu dola bilioni 671.9 ifikapo mwaka 2030 endapo kasi ya ukuaji wa sasa itaendelea.
Taifa la Saudi Arabia, lililoingiza watalii milioni 18.5 mwaka 2024 pekee, ndilo linaloongoza kwa kuvuna soko la utalii wa kidini kupitia ibada za Hijja na Umra kwa Waislamu, huku India ikifuatia, kisha Italia na Hispania.
Tanzania ina fursa lukuki za utalii wa kidini. Kwa upande wa dini ya Kiislamu, kuna Msikiti Mkuu wa Kilwa Kisiwani uliojengwa katika karne ya 12.
Huo ni miongoni mwa misikiti ya zamani Afrika Mashariki, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Fursa nyingine ni Msikiti wa Kizimkazi visiwani Zanzibar, wenye maandishi ya Kiarabu ya karne ya 12. Pia kuna Msikiti wa Malindi, Stone Town visiwani humo, wenye historia ya biashara ya Waarabu na Uislamu.
Bagamoyo ni fursa nyingine ya utalii wa kidini, kwa kuwa ina historia ya kuwa kituo muhimu cha elimu ya Kiislamu na biashara ya karne ya 19.
Kwa upande wa fursa za utalii wa dini ya Kikristo, Bagamoyo mkoani Pwani kuna Kanisa Katoliki la kwanza Afrika Mashariki na makumbusho ya wamisionari.
Pia kuna Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam, ambalo ni urithi wa Kilutheri wa Wajerumani, huku Kipalapala mkoani Tabora kukiwa na seminari ya kwanza ya Katoliki Tanzania.
Peramiho mkoani Ruvuma kuna kituo kikubwa cha Kanisa Katoliki, huku Lugala mkoani Kigoma kukiwa na urithi wa wamisionari wa karne ya 19.
Pamoja na fursa zote hizo, idadi ya watalii wanaokuja nchini kwa madhumuni ya utalii wa kidini ni asilimia 0.02 pekee, kwa mujibu wa Ripoti ya Wageni wa Kimataifa Wanaoingia Tanzania ya mwaka 2023.
Asilimia 86 huja kutalii kwa likizo na mapumziko na hutembelea zaidi hifadhi za Taifa.
Zungu ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma leo, Ijumaa, Februari 6, 2026, alipozungumza kuhitimisha mjadala wa Kamati ya Mipango ya wizara mbalimbali.
Amesema Tanzania ilibahatika kuwa na Kiongozi Mkuu wa Katoliki, Papa Leo, aliyeishi Tanzania katika maeneo ya Zanzibar, Morogoro, Songea na Dar es Salaam.
“Hivi tukiweka maeneo ya kumbukumbu za historia za kidini, shida iko wapi? Wanakuja wageni wengine si Wakristo; wanakuja kutazama Papa Leo Morogoro alikuwa anakaa nyumba gani, kanisa alilokuwa anasali Songea,” amesema.
Amesema watafutwe marafiki waliokuwa karibu naye na pengine inawezekana hata gari alilokuwa anaendesha lipo, vyote hivyo vitumike kuwa fursa ya utalii.
Ametolea mfano Misri yenye watalii milioni 19 wanaokwenda kutazama majengo ya Mafarao na vitu vyao, akizingatia hawakuwa na dini yoyote.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii lazima ichangamke, akimsihi Waziri Mkuu (Dk Mwigulu Nchemba) akafanyie kazi hoja hiyo kwa kutafuta mtaalamu ili kupata watalii wasiopungua milioni nne kwa mwaka.
“Kuna Waislamu wakitoka Umra hawataki kurudi makwao; wanaweza kuja Kilwa, Bagamoyo, Zanzibar. Hoja ile ya zamani mnaleta mambo ya udini — hakuna mambo ya dini kwenye fedha,” amesema.
Ameeleza mipango ya Serikali inahitaji fedha na si maneno wala nyimbo, hivyo ni vema Waziri Mkuu akae na wataalamu kuondoa misuguano isiyo na msingi.
Katika ufafanuzi wake, amesema Tanzania ina watu wenye mitazamo ya kizamani kwamba ukiwaambia jambo wanasema zamani halikufanyika, ilhali vijana wa sasa wanataka mambo yanayofanywa kwa ajili ya leo na kesho.
“Kweli wabunge hawa tutabanana kweli kweli humu ndani. Sheria zetu bado si rafiki kwa uwekezaji, si rafiki kabisa. Zote tunalinda hiki, mtu anashindwa kusoma andiko, kimbilio lake la kwanza ni kusema: hapa kuna usalama, hapa kuna hiki…
Tutapambana mpaka hiki kitu kiende mbele. Serikali ichukue ifanyie kazi. Watu watapenda kuona Papa Leo alisali wapi, alikaa wapi, benchi gani alikuwa anakaa,” amesema.
Amewataka Waziri Mkuu na viongozi wengine wakae na kulichakata jambo hilo, akiwasihi watu waondokane na mitazamo ya kizamani, roho mbaya na fitina, na kwamba mtu akifuatilia jambo asionekane ana maslahi binafsi ndani yake.
“Mimi nimepata bahati nimeishi kwenye makundi yote hayo, nina ujana zaidi ya vijana. Sijabadilika mimi,” amesema.
Mtaalamu wa mikakati ya utalii, Dk Amini Keka, amesema iwapo Serikali itafanyia kazi, itasaidia kuipa Tanzania uthabiti wa mapato ya utalii.
“Utalii wa kidini ni utalii wa mahitaji ya kudumu; waumini husafiri bila kujali misimu. Hii itasaidia kupunguza utegemezi wa utalii wa wanyamapori pekee na kuongeza mapato ya taifa kwa mtiririko wa uhakika mwaka mzima,” amesema.
Mwekezaji katika huduma za malazi na usafiri wa kitalii, Neema Salum, amesema utalii wa dini utakuwa kichocheo cha uwekezaji wa ndani.
“Tofauti na aina nyingine za utalii, utalii wa kidini huvutia makundi makubwa kwa wakati mmoja, hali inayotoa uhakika wa soko kwa hoteli, usafiri na biashara ndogondogo. Serikali ikitoa mwelekeo sahihi, mitaji binafsi itafuata,” amesema.
Mdau na mtafiti wa masuala ya urithi wa Taifa, Mwakalinga James, amesema thamani ya kijamii na kihistoria ya sekta hiyo ipo katika utalii wa kiroho, yaani kidini.
“Kuwekeza kwenye utalii wa kidini si biashara pekee; ni uwekezaji wa kulinda kumbukumbu za Taifa. Bila mkakati wa makusudi, maeneo mengi ya kihistoria na kiroho yataendelea kusahaulika pamoja na fursa za elimu, ajira na utambulisho wa Tanzania kimataifa,” amesema James.