Baba asimulia alivyowaokoa wanawe wawili moto ukiteketeza nyumba

Tanga. Baba wa watoto wawili, Hansi Mohamed, mkazi wa Mtaa wa Majengo Mapya, Kata ya Mzingani jijini Tanga, amesema amepitia wakati mgumu kumuokoa mwanawe wa miaka minne katika tukio la moto, huku akiwa amembeba mtoto wake mwingine wa miezi sita mikononi.

Tukio hilo la moto lilitokea jana Ijumaa Februari 6, 2026 na kuteketeza mali zote zilizokuwapo ndani ya nyumba hiyo, na kuwaacha wapangaji wakiwa hawana mahali pa kuishi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 7, 2026, Mohamed amesema wakati tukio hilo linatokea alikuwa nje ya nyumba, alipouona moto na moshi mzito ukitanda ghafla. Amesema alikuwa na watoto wawili, mmoja wa miaka minne na mwingine wa miezi sita, huku mtoto wa miaka minne akiwa ndani ya chumba ambacho moto ulianzia.

“Nilipoona moshi mzito, ilibidi niongeze ujasiri niingie ndani kumkimbilia mtoto wa miaka minne, nikiwa nimembeba yule wa miezi sita mikononi,” amesema Mohamed.

Ameongeza kuwa alipofanikiwa kuingia ndani, alimkuta mtoto huyo akihangaika, akamshika mkono na kwa kushirikiana na majirani waliokuwapo akafanikiwa kutoka naye nje salama.

Muonekano wa nyumba iliyotekelea moto  katika mtaa wa Majengomapya  kata ya Mzingani jijini Tanga.



Mohamed amesema wapangaji wa nyumba hiyo wamepoteza mali zao huku akiiomba Serikali iwasaidie.

“Tumepoteza kila kitu. Tunashukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu familia zetu zote zimetoka salama, lakini tunaomba msaada kwa mali tulizopoteza, baadhi yetu ni wafanyabiashara na hatukufanikiwa kuokoa chochote,” amesema.

Kwa upande wake, Mariamu Stambuli, mpangaji wa nyumba hiyo, amesema ameshuhudia mali zake zikiteketea huku akishindwa kuokoa hata kitu kimoja.

Mmiliki wa nyumba hiyo, Omary Abdi, amesema alipata taarifa za tukio hilo akiwa kwenye shughuli zake na alipofika eneo la tukio, alikuta nyumba yote iliyokuwa na vyumba sita ikiwa imeteketea.

“Hakuna mpangaji aliyefanikiwa kuokoa mali yoyote, isipokuwa banda la uwani ambalo halikuathirika,” amesema Abdi.

Wapangaji wa nyumba iliyounguwa kwa moto  katika mtaa wa Majengomapya kata ya Mzingani jijini Tanga wakiwa nje.



Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Luka Mwanga, amesema walipofika eneo la tukio walifanikiwa kuuzima moto lakini tayari mali zilikuwa zimeteketea zote.

“Hatukukuta majeruhi. Tumeokoa nyumba za jirani kwa asilimia 100, na tunatoa pongezi kwa wananchi kwa kushirikiana nasi katika kukabiliana na moto huo,” amesema Mwanga.

Amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakati wa majanga, huku akiwahimiza wamiliki wa majengo kufanya ukarabati wa mara kwa mara, hususan majengo ya zamani, ili kuepuka matukio ya moto yanayosababishwa na hitilafu za mifumo ya umeme.

Kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.