DC Itunda Ahimiza chakula mashuleni Mbeya

📍 Ammwagia sifa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuboresha miundombinu

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

MABORESHO yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya elimu yameendelea kuzaa matunda baada ya ufaulu wa wanafunzi kuongezeka kwa kasi nchini. 

Akizungumza na wadau wa elimu Jijini hapa, Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe Solomon Itunda alisema maboresho katika sekta ya elimu yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufaulu nchini.

Itunda alisema hatua hiyo imetokana na  uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, maabara, na uboreshaji wa mazingira ya kufundishia, jambo ambalo limerejesha hamasa ya kusoma kwa wanafunzi na walimu.

Alisema katika kuyaenzi maboresho hayo na kuhakikisha tija inaonekana darasani, Mkuu huyo wa wilaya amewaeleza wadau wa elimu Jijini Mbeya kwamba ni vema kuweka mkakati wa kudumu wa ustawi wa wanafunzi ikiwemo kuhakikisha kila shule watoto wanapata chakula cha mchana kuboresha afya ya Mwanafunzi.

Hivyo, Mkuu huyo wa wilaya akawaagiza  Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa kuhakikisha kila mzazi na mlinzi anatimiza wajibu wake wa kuchangia chakula shuleni. 

“Serikali imeshajenga madarasa na kuboresha mazingira; wajibu wa mzazi ni kuhakikisha mtoto ana nishati ya kusoma. Watendaji msimame imara, wazazi watakaokaidi agizo hili wachukuliwe hatua mara moja,” alisisitiza Mhe. Itunda.

Mbali na lishe, kikao hicho kimepitisha mikakati mipya ya kupandisha kiwango cha ufaulu ndani ya Jiji la Mbeya kwa kuimarisha usimamizi wa taaluma na ujenzi wa ushirikiano wa “pande tatu” kati ya walimu, wazazi, na viongozi wa mitaa. 

Pia Mkuu huyo wa wilaya amewapongeza walimu wa shule za za Jiji la Mbeya kwa uzalendo wao na kazi kubwa ya kulea taifa, akiwataka wasirudi nyuma katika jukumu hilo takatifu.

Akihitimisha, Mkuu wa Wilaya amemshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu na uimarishaji wa maslahi ya walimu ambao wamepelekea  Jiji la Mbeya kuimarika kielimu, na kuahidi kuwa wilaya yake itahakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo ya daraja la kwanza kwa kila mwanafunzi.

DC Itunda ahimiza chakula mashuleni Mbeya