Mastaa Yanga wawekewa mkwanja mrefu Morocco

KUNA ujumbe mfupi sana wachezaji wa Yanga wamepewa na bilionea wao Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ na kama wakishinda tu basi hamnahamna kila staa ataondoka na sio chini ya Sh40-50 milioni, lakini yule winga mpya amekwama buana.

Mastaa wa Yanga wamepokea ujumbe wa tajiri wao GSM ambaye kama ambavyo ukikutana naye ukimuuliza swali atakwambia “Yanga Bingwa”, basi hapa nako hakutaka maneno yawe mengi, akawaambia tu, nendeni mkashinde “bilioni moja yenu”.

Ahadi hiyo imewapa mzuka sana wachezaji wa Yanga ambapo nao wakaliamsha kwa kukaa kikao cha wenyewe kwa wenyewe wakijipanga na mchezo huo wa leo dhidi ya AS FAR Rabat.

Iko hivi; Yanga kama itashinda leo itaweka rekodi ya mara ya kwanza kufuzu kwenda robo kabla ya mchezo wa mwisho, lakini ahadi hiyo ya fedha ndio imewaamsha zaidi na kuanza kuwapigia hesabu kubwa Waarabu hao.

YANG 03


“Tajiri ukiondoa salamu yake hajaongea sana kaka, kama kawaida yake amesema maneno haya tu ‘kashindeni bilioni moja yenu nawapa,’ aisee huku tutauana haitakuwa rahisi kabisa kwao,” amesema staa mmoja ndani ya kikosi hicho cha Wananchi.

Hesabu nyingine za Yanga zimetibuka kimtindo baada ya winga wake mpya Buba Jammeh kukwama kutua nchini Morocco kuungana na kikosi cha timu hiyo.

Yanga baada ya usajili wa winga huyo mpya ilikuwa inataka akaungane na wenzake nchini humo kabla ya mchezo wa leo dhidi ya wenyeji wao AS FAR Rabat lakini mambo yamekwama.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Buba ameshindwa kupata visa kwa wakati akitokea Angola ili atue nchini Morocco kama ambavyo kocha wa  timu hiyo Goncalves alikuwa akitaka hesabu hizo.

YANG 01


Yanga baada ya kukwama huko imebadilisha hesabu hizo ambapo Buba sasa ataanza taratibu za kuja nchini akitarajiwa kutua mapema wiki ijayo.

“Kule Angola ndio mambo yamekwama, tulikuwa tunataka apate visa ya kwenda Morocco moja kwa moja lakini mpaka jana (juzi) wametujulisha imeshindikana bado hawajapitisha hati hiyo,” amesema bosi huyo.

“Hata kama angekuja basi angefika leo (jana) isingekuwa rahisi kuweza kufanyika lolote ili acheze maana hata wenzake watakuwa wameshafanya mazoezi ya mwisho, tumeona asije tena huku tutakutana naye Tanzania nadhani mpaka Jumatatu ijayo atakuwa hapa.

YANG 02


“Mashabiki wana kiu tunaona wanavyoulizia lakini kocha wetu (Pedro) ndio ameumizwa sana kwa kuwa yupo kwenye mahitaji yake zaidi yetu kwa ajili ya sababu za kiufundi, tunachoshukuru ameelewa yaliyokwamisha.”

Aidha, Yanga inaamini kwa kikosi walichosafiri nacho kinaweza kuwapa matokeo mazuri katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay, ambao hautahudhuriwa na mashabiki kutoka na wenyeji hao kutumikia adhabu.

“Bado tuna imani kwamba kikosi chetu ambacho kimesafiri kipo imara na tunaweza kupata ushindi kwenye mchezo huu mgumu.” amesema bosi huyo wa miamba ya soka Tanzania.