Mauwasa yaanza kufunga mita za maji za malipo kabla

Maswa. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) imeanza kufunga mita za maji za mfumo wa malipo ya kabla (prepaid water meters) kwa wateja wake.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 7, 2026, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Kassim Kado amesema hatua hiyo inalenga kuboresha uwajibikaji, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuhakikisha wateja wanapata huduma ya maji kwa haki na kwa gharama halisi kadiri wanavyoyatumia.

Amesema kupitia mfumo wa mita hizo, mteja atalipa maji kulingana na matumizi yake bila kukabiliwa na makadirio yasiyo sahihi ya bili.

“Utekelezaji wa agizo hilo utaondoa migogoro ya mara kwa mara kati ya wateja na mamlaka kuhusu bili kubwa za maji, huku ukisaidia kudhibiti upotevu wa mapato na matumizi mabaya ya rasilimali ya maji,” amesema.

 Mauwasa imewahakikishia wateja kuwa kazi ya ufungaji wa mita hizo itaendelea sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi, huku ikiahidi kuboresha huduma ya maji kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali na maslahi ya wananchi.

Angelina Masalu, mkazi wa Uzunguni mjini Maswa, amesema mfumo wa mita hizo utasaidia kuondoa usumbufu uliokuwepo kwa muda mrefu.

 “Kwa kweli huu ni uamuzi mzuri sana. Tumekuwa tukipata bili kubwa ambazo hazilingani na matumizi halisi. Mfumo wa mita hizi utatusaidia kujua matumizi yetu na kupanga bajeti bila presha,” amesema.

Mkazi mwingine, Catherine Daniel amesema utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuwasikiliza wananchi wa kawaida.

“Mara nyingi tulikuwa tunalalamika lakini hatupati majibu ya haraka. Hii inaonesha Rais Samia anawajali wananchi. Tukilipa kulingana na matumizi yetu, haki itapatikana,” amesema.

Mkazi mwingine, Slivester Mutegeki ameitaka Mauwasa kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya mita hizo ili kuepusha changamoto mpya.

“Mfumo ni mzuri lakini elimu ni muhimu. Kuna wananchi bado hawajazoea hizi mita. Mauwasa watoe elimu ya kutosha ili mfumo huu uwe na manufaa kwa wote,” amesema Mutegeki.