Geita. Shule za sekondari ya Evarist iliyopo Kata ya Nyarugusu na Rwamgasa, Kata ya Rwamgasa, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, zimepatiwa baiskeli zitakazowawezesha wanafunzi kuwahi masomo kwa wakati.
Jumla ya baskeli 100 zimetolewa, kila shule imepokea 50 kupitia ufadhili wa Mgodi wa Mwamba Mining kwa kushirikiana na Asante Africa Foundation pamoja na Buffalo Bicycles, ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau hao katika kuinua sekta ya elimu kwa wananchi waishio vijijini.
Baadhi ya wanafunzi katika shule hizo walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita nne hadi nane kila siku kufika shuleni, hali iliyowalazimu kupita katika mashamba na maeneo yasiyo salama.
Akikabidhi baskeli hizo leo Jumamosi Februari 7, 2026, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Lucy Beda amewashukuru wadau kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu, hususan katika maeneo yanayozunguka migodi.
Beda amesema mazingira ya uchimbaji huwakwamisha baadhi ya wanafunzi kuendelea na masomo kutokana na umbali wa shule na kuwafanya kuvutiwa na shughuli za uchimbaji badala ya elimu. Ameongeza kuwa baiskeli hizo zitapunguza uchelewaji wa wanafunzi na kuongeza umakini darasani.
Amesema ufadhili huo unawalenga wanafunzi wanaoishi umbali wa zaidi ya kilomita nne kutoka shuleni, hususan wasichana wa kidato cha kwanza na cha pili, akitolea mfano wanafunzi kutoka vijiji vya Buziba, Busolwa na Ikindu.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Yohana Katambi amewataka wazazi na walimu kushirikiana katika kutunza baiskeli hizo ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Diwani wa Nyarugusu, Daniel Shilogela amewasihi wazazi kuzithamini baskeli hizo na kuhakikisha zinatumiwa na wanafunzi waliokusudiwa pekee, huku Meneja wa Mgodi wa Mwamba Mining, Calvin Habil, akisisitiza uwazi na haki katika ugawaji wake.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Evarist wameshukuru kwa msaada huo na kuahidi kuongeza bidii katika masomo ili kuboresha matokeo yao ya kitaaluma.