Nchimbi: Mageti ya Ikulu yafungwe dhidi ya waovu

Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania wa dini zote kutumia nafasi yao ya kiimani kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa afya, busara na usalama wake vina uhusiano wa moja kwa moja na utulivu, mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Mbali na hilo amesema kuna haja pia ya kumuombea Rais apate wasaidizi waaminifu, wa kweli na wenye uzalendo wa dhati, watakaotanguliza masilahi ya Taifa badala ya binafsi.

Dk Nchimbi amesema hayo jana Ijumaa Februari 6, 2026 wakati wa hafla ya kusimikwa Uongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPTC), iliyofanyika katika Ukumbi wa Agape Life Church jijini Dar es Salaam.

Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kutambua nafasi nyeti ya Rais katika uendeshaji wa nchi, akieleza kuwa, bado wapo baadhi ya watu wasiouelewa uzito wa nafasi hiyo na athari zake kwa Taifa kwa jumla.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini, mliombee Taifa letu lakini pia nawaomba muendelee kumuombea Rais wetu. Wako watu ambao hawajui umuhimu wa nafasi ya Rais katika nchi. Kuna wanaofikiri Rais akipata shida nchi haipati shida,” amesema Dk Nchimbi.

Makamu wa Rais alirejea maneno ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuwa, “unaweza kumtikisa mtu yeyote katika jamii, nchi ikaendelea kuwa tulivu, lakini ukimtikisa Rais, Taifa lote hutikisika.”

Katika hotuba yake, Dk Nchimbi amesema maombi kwa ajili ya Rais si jambo la hiyari, bali ni wajibu wa kitaifa na kiimani na kuwasisitiza viongozi wa dini kuwa wana wajibu wa kuliombea Taifa kama ilivyoelekezwa kwenye Biblia na hawapaswi kuchoka kufanya hivyo.

“Ukimgusa Rais, nchi inatikisika. Ndiyo maana ni lazima tumuombee Rais wetu kila siku afya njema na maisha marefu ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu, lakini pia kumuombea busara na hekima ziendelee kumiminika kwake katika uamuzi anaoufanya kwa masilahi ya Taifa ,” amesisitiza.

Hata hivyo, ameonya juu ya uwepo wa watu wenye nia ovu wanaoweza kujaribu kupenyeza ushauri mbaya au njama ndani ya mifumo ya uongozi, akisisitiza umuhimu wa maombi ili kumkinga Rais dhidi ya watu wa aina hiyo.

“Tuendelee kumwomba Mungu aweze kumsaidia kupata wasaidizi waaminifu na wa kweli. Apate wasaidizi wanaoipenda nchi yetu kwa kweli, wanaoumwa na maendeleo ya nchi yetu, wanaotamani nchi yetu ibadilike na iwe bora zaidi na zaidi,” amesema.

“Tumuombe Mwenyezi Mungu ampe Rais ‘macho ya tai’ ili aweze kuwaona na kuwatambua watu wabaya, wachonganishi, wafitini, waongo, wezi na wote wasio waaminifu.

“Pia, tumuombe Mungu afunge mageti ya Ikulu dhidi ya watu wabaya. Kupitia maombi yenu, watu wote ambao wana mawazo ya wizi, ubadhilifu, uchonganishi, na hata mawazo ya kumwaga damu za watu, waone Ikulu hapaingiliki kwa namna yeyote ile,” amesema.

Ameongeza kuwa watu wenye nia mbaya wasitamani hata kusogea karibu na Rais, wala kupata fursa ya kumshauri vibaya kiongozi huyo mkuu wa chini na Serikali.

“Nataka watu wote wanaoamini katika dini wamuombee Rais wetu. Tufunge mageti ya Ikulu, wasipenye watu wabaya wanaokwenda kumshauri vibaya Rais,” amesema.

Akizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema maombi ya makamu wa Rais kwa viongozi wa dini ni ya  msingi kwa sababu urais ni taasisi na taasisi inaweza kuwa kokoro linalovuta watu wema na wabaya.

 “Urais unatia upofu na ukiziwi. Kwa hiyo ni muhimu kumwomba Mungu amsaidie Rais asipate upofu wala ukiziwi ili aone na kusikia. Watu wabaya wasikaribie ikulu yetu. Mungu amjalie hekima kutambua kuwa walipo 12 kuna Yuda. Na kwamba hata katika nguo zake anaweza kuwamo chawa anayemsumbua kwa sababu kikulacho ki nguoni mwako. Taifa liombewe na Rais aombewe.”

Askofu Bagonza amesema pamoja na maombi yote, mwisho wa siku, Rais anasimama peke yake mbele za Mungu kutoa hesabu juu ya Taifa na hapo hawezi kusema mambo fulani yalifanywa na washauri au wasaidizi.

“Ni rais peke yake tu. Akishauriwa vibaya akakubali hana tena nafasi ya kujitetea. Ni yeye aliapa na ni yeye anayetoa hesabu mbele za muumba. Aombewe ili atambue wajibu huu uliowekwa mikononi mwake si mikononi mwa washauri.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Rashid Nkya amesema wito wa kumuombea Rais una mizizi katika historia ya Tanzania kama Taifa lenye mshikamano wa kidini huku akisisitiza kuwa, kuna umuhimu wa kuunganisha maombi, maadili, mifumo thabiti ya utawala bora na uwajibikaji wa viongozi ili kulinda masilahi ya Taifa.

Amesema ujumbe huo wa Makamu wa Rais unalenga kuimarisha umoja wa kitaifa na kuwakumbusha wananchi uzito wa nafasi ya Rais katika utulivu wa nchi.

“Katika mazingira yenye changamoto za kiusalama na kiuchumi duniani, kuhimiza mshikamano wa kiimani ni njia ya kuimarisha matumaini na utulivu wa jamii,” amesema.

Nkya amesema kwa upande mwingine kauli ya Dk Nchimbi imebeba ujumbe mzito wa kisiasa unaopaswa kutafsiriwa kwa umakini.

Amesema wito wa kumuombea Rais kupata wasaidizi waaminifu ni ishara ya kukiri kuwa changamoto kubwa katika uongozi mara nyingi hazitokani na kiongozi mmoja, bali mfumo mzima wa washauri na watendaji.

“Hata hivyo, maombi yanapaswa kwenda sambamba na mifumo imara ya uwajibikaji na uwazi,” amesisitiza.

Mtaalamu wa sayansi ya siasa, Rehema Kitope amesema ingawa kumuombea Rais ni jambo jema kijamii na kiimani, msingi wa utawala bora haupaswi kuegemezwa kwenye maombi pekee.

Amesema kusisitiza maombi ya kumlinda Rais dhidi ya watu wabaya kunapaswa pia kuambatana na kuimarisha taasisi za usalama na haki kwa kile alichoeleza, usalama wa Taifa unajengwa zaidi kwa mifumo imara ya kisheria na kitaasisi.

“Demokrasia imara inahitaji wananchi wanaouliza maswali, taasisi huru na mifumo ya uwajibikaji, sambamba na imani binafsi. Kama taasisi zinafanya kazi ipasavyo, nafasi ya njama na ushauri mbaya inapungua kwa kiasi kikubwa,”amesema Rehema.