AKIWA amehusika na pointi 14 kati ya 19 ilizoivunia Namungo, mshambuliaji Fabrice Ngoy amesema mafanikio ya ubora yanatokana na kuamini katika kujaribu na ushirikiano uliopo kati yake na wenzake.
Ngoy, ambaye amefunga mabao sita sawa na kinara wa Ligi Kuu kwa sasa, Saleh Karabaka wa JKT Tanzania, ameandika rekodi ya kufunga mabao muhimu kwa Namungo ambayo yamezalisha pointi 14 kati ya 19 ilizokusanya timu hiyo.
Mechi alizofunga Ngoy ni dhidi ya Tanzania Prisons (1-0, pointi 3), Azam FC (1-1, pointi 1), Mbeya City (1-0, pointi 3), Coastal Union (1-0, pointi 3), KMC (1-0, pointi 3) na Fountain Gate (1-1, pointi 1).
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoy amesema hawezi kuwa bora bila wachezaji wenzake 10 uwanjani, hivyo anaamini ushirikiano mzuri walionao ndio siri ya mafanikio wanayoyapata chini ya kocha Juma Mgunda.
“Najivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya timu yangu. Nitapambana hadi mwisho kuhakikisha tunafikia malengo. Namshukuru kocha Mgunda kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza mbele ya wachezaji wengine bora waliopo Namungo,” amesema Ngoy.
“Natumia fursa hii kuonyesha kuwa nafasi ninayopewa nastahili, lakini pia napambania timu iweze kufikia malengo kwa kujaribu kutumia kila nafasi ninazotengenezewa. Lengo ni kuona tunakwepa changamoto ya kushuka daraja au kumaliza katika nafasi mbaya kwenye msimamo.”
Ngoy, akizungumzia ligi kwa ujumla na mpango wake msimu huu katika kufumania nyavu, amesema atafunga kila atakapopata nafasi na hayupo tayari kuweka idadi ya mabao atakayofunga, kwani anaweza kuvuka idadi atakayotaja au akashindwa kufikia.
“Kufunga siyo bahati, ni kutumia nafasi. Hivyo sipo tayari kutaja ni idadi gani ya mabao natamani kufunga msimu huu. Ahadi yangu ni kufunga kila nitakapopata nafasi ili kuisaidia timu kufikia malengo,” amesema.
“Ligi ni ngumu sana msimu huu; timu zimejipanga kutokana na sajili zilizofanywa, hivyo mikakati sahihi ya wachezaji na benchi la ufundi ndio itakayotufanya tuweze kufikia malengo. Nitapambana kwa kushirikiana na wenzangu kuhakikisha Namungo inakuwa bora na timu tishio msimu huu.”