Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela alichokuwa amehukumiwa Konstebo wa Polisi, Emmanuel Manase baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa na uzito wa kilo 208.15.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka, ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika hatua za kipelelezi pamoja na Mahakama iliyomtia hatiani kushindwa kuchambua ushahidi kwa kina.
Uamuzi uliomuachia huru Manase ulitolewa jana Ijumaa Februari 6, 2026 na jopo la majaji watatu ambao ni Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Deo Nangela, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo namba 490/2023 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Kairo amesema baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, Mahakama imekubaliana kuwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani mrufani huyo ulikuwa na dosari kubwa za kisheria.
Dosari hizo ni pamoja na ushahidi wa vielelezo uliokiuka taratibu, ushahidi unaokinzana kuhusu gari lililodaiwa kutumika kusafirisha bangi hiyo, pamoja na kuvunjika kwa mnyororo wa uhifadhi wa dawa za kulevya zilizokamatwa.
Kutokana na dosari hizo, Mahakama ilifuta hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Julai 14, 2023 na kuamuru mrufani aachiliwe huru isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.
Awali, mrufani aliyekuwa Konstebo wa Polisi, alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na alikamatwa Mei 22, 2020 katika eneo la Mzunguko wa Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, akiwa na kilo 208.15 za bangi ndani ya gari aina ya Toyota Harrier, iliyokuwa na namba za usajili T 129 DPC.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi tisa na vielelezo vinane likiwamo gari lililodaiwa kukutwa na dawa hizo za kulevya, majani makavu yaliyokuwa kwenye mifuko 12 ya salfeti.
Ilidaiwa siku ya tukio asubuhi, mrufani alikamatwa baada ya kupatikana taarifa kuwa kulikuwa na magendo yaliyosafirishwa kupitia Barabara ya Msata–Bagamoyo na baada ya upekuzi kufanyika mbele ya mashahidi huru, mrufani alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Bagamoyo mkoani Pwani.
Ilidaiwa baada ya majani hayo kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) kwa ajili ya uchambuzi, ilibainika yalikuwa ni bangi yenye uzito wa kilo 208.15.
Katika utetezi wake, mrufani alikana kutenda kosa hilo na kudai siku ya tukio aliripoti kituo chake cha kazi, Kituo cha Polisi Vigwaza akiwa kwenye gari lake binafsi aina ya Toyota Harrier.
Alidai baadaye aliagizwa kuripoti Kituo cha Polisi cha Bagamoyo, alienda kwa kutumia usafiri wa umma na alipofika na kukutana na aliyepaswa kumuona kituoni hapo, alimtuhumu kwa kuchelewa.
Mrufani alidai kuwa aliambiwa amesababisha hasara kwa wadau wake akiwamo mkewe katika biashara yao ya mafuta ya kupikia kwa kuwakamata na kuwapeleka TRA.
Alieleza kuwa kutokana na madai hayo, aliwekwa kizuizini na baadaye alitakiwa kwenda kuchukua gari lake Kituo cha Polisi Bagamoyo na kulikabidhi pamoja na funguo zake kwa ASP Maleko.
Mrufani huyo alidai kukaa rumande hadi Juni 8, 2020, alipelekwa katika Ofisi ya OCD na kuarifiwa kuhusu kosa la kutotii amri za juu na kufukuzwa kazi bila kusikilizwa, kisha akashtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.
Baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, mrufani alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Katika rufaa hiyo, mrufani alijiwakilisha mwenyewe Mahakamani bila kuwa na wakili huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili wa Serikali wawili, ambao waliunga mkono rufaa hiyo na kueleza kuwa kesi haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Mrufani huyo alikuwa na sababu sita za rufaa ikiwamo tofauti kati ya taarifa na ushahidi uliotolewa, kutegemea vielelezo halisi ambavyo havikuorodheshwa au kuelezewa kwa mrufani, kutegemea ushahidi usioendana na unaopingana na kuwa kesi dhidi yake haikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Baada ya kupitia hoja za pande zote pamoja na mwenendo wa kesi, Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa gari lililotumika kama kielelezo muhimu katika kesi hiyo liliwasilishwa na kutegemewa katika kumtia hatiani mrufani, licha ya kutokuwa sehemu ya orodha ya vielelezo vilivyotajwa wakati wa kesi ya kukabidhiwa dhamana.
Kwa mujibu wa Mahakama, kitendo hicho kilikiuka masharti ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kumweka mrufani katika hali ya kushtukizwa na kuwa kutokana na ukiukwaji huo, Mahakama iliamua kupuuza kabisa ushahidi unaohusiana na gari hilo ikisema haukuwa halali kisheria.
Jaji amesema Mahakama pia ilibaini mkanganyiko mkubwa kati ya shtaka na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kuhusu gari lililodaiwa kutumika kusafirisha bangi na kuwa, wakati kwenye shtaka ilidaiwa mrufani alitumia gari lenye namba ya usajili T 129 DPC aina ya Toyota Harrier.
Ila mashahidi wa mashtaka walieleza kuwa bangi ilipatikana kwenye gari lenye namba T 619 DEQ na uchunguzi wa baadaye ulionyesha namba hiyo ya pili ilikuwa ya gari aina ya Toyota Noah, si Harrier.
Mahakama ilisema tofauti hiyo ilienda moja kwa moja kwenye kiini cha kesi na kwa kuwa upande wa mashtaka haukufanya marekebisho ya shtaka, ushahidi huo haukuwa na uwezo wa kuthibitisha kosa.
Kuhusu suala la mnyororo wa uhifadhi wa bangi iliyodaiwa kukamatwa, Mahakama ilibaini kulikuwa na upungufu mkubwa wa namna mifuko 12 ya bangi ilivyoshughulikiwa kuanzia ilipokamatwa hadi ilipowasilishwa Mahakamani.
Majaji walibaini kuwa bangi hiyo haikuwekewa lebo, haikupimwa wala kupigwa picha wakati wa kukamatwa na rekodi za uhamisho wa ushahidi kutoka ofisa mmoja hadi mwingine zilikuwa hazieleweki na kulikuwa na ushahidi unaokinzana kuhusu ni nani aliyekuwa na bangi hiyo katika hatua mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mahakama, upungufu huo ulivunja mnyororo wa ulinzi wa ushahidi na kuacha uwezekano wa ushahidi kuchezewa au kubadilishwa, hali iliyoufanya ushahidi huo kutokuwa wa kuaminika.