NYOTA mpya wa Simba SC, Anicet Oura, amefanikiwa kufunga bao lake la kwanza akiwa na kikosi cha timu hiyo baada ya kujiunga nacho dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea IF Gnistan ya Finland.
Winga huyo amefunga bao moja katika sare ya 1-1 iliyopata Simba dhidi ya Petro Atletico, ikiwa ni mechi ya tano Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi hiyo iliyochezwa leo Jumamosi Februari 7, 2026 kwenye Uwanja wa 11 de Novembro uliopi Luanda nchini Angola, Simba ilikuwa ni sehemu ya kuelekea kukamilisha ratiba lakini wapinzani wao walihitaji zaidi ushindi kujiweka sehemu nzuri ya kufuzu robo fainali.
Mapema dakika ya 13, Pedro Pinto aliitanguliza Petro Atletico alipofunga bao kupitia pasi ya Benny Dias, bao ambalo liliibua matumaini ya wenyeji hao katika kuwania kufuzu robo fainali.
Matumaini zaidi yalikuja dakika ya 40, baada ya beki na nahodha wa Simba, Shomari Kapombe kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu na kuwafanya vijana hao wa Steve Barker kucheza pungufu ya mchezaji mmoja.
Mapema kipindi cha pili, Barker akafanya mabadiliko, akamtoa kiungo Morrice Abraham na kumuingiza beki David Kameta ‘Duchu’ ili kuimarisha ulinzi kufuatia kuwa pungufu eneo hilo baada ya Kapombe kuonyesha kadi nyekundu.
Dakika ya 51, Barker alifanya mabadiliko mengine ya wachezaji watatu, akiwatoa Kibu Denis, Allasane Kante na Elie Mpanzu, wakaingia Seleman Mwalimu, Inno Loemba na Anicet Oura.
Mabadiliko hayo yalikuja kujibu dakika ya 81, baada ya Oura kupokea pasi akiwa katikati ya uwanja na kummegea pande Mwalimu upande wa kulia, kisha akapiga krosi kati iliyomalizia vizuri na Oura, akiisawazishia Simba.
Bao hilo liliibua shangwe si tu kwa wachezaji waliokuwa wakipongezana, bali hata watu wa benchi la ufundi la Simba wakiongozwa na Barker na msaidizi wake, Seleman Matola.
Kabla ya bao hilo, dakika ya 79 Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Antony Mligo na kuingia Naby Camara.
Petro Atletico nayo katika kusaka bao la pili, ilifanya mabadiliko kwa nyakati tofauti kipindi cha pili kwa kuwatoa Antonio Hossi, Jonathan Toro, Tiago Reis, Costinha na Augusto Ilidio, wakaingia Anderson Cruz, Maya, Joaquim Paciencia, Vanilson na Julinho.
Sare hiyo imeifanya Simba kufikisha pointi mbili ikiendelea kukaa mkiani mwa kundi D, huku Petro Atletico ikiwa nafasi ya tatu ikikusanya pointi sita.
Simba itafunga hesabu wikiendi ijayo itakapoikaribisha Stade Malien kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, wakati Petro Atletico ikiifuata Esperance nchini Tunisia.