CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeanza rasmi Awamu ya Pili ya Programu ya Msingi ya Sayansi kwa wanawake wanaotoka katika mazingira magumu kwa mwaka wa masomo 2025/2026, mkoani Singida.
Programu hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kuratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Lengo kuu ni kuwapatia wanawake waliokosa fursa ya awali ya kusoma masomo ya sayansi, msingi imara wa kitaaluma, kujiamini na maarifa yatakayowawezesha kuendelea na elimu ya juu pamoja na kufanikisha ndoto zao za kitaaluma.
Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanajengewa misingi madhubuti katika masomo ya sayansi kama hatua ya maandalizi ya kuendelea na masomo ya juu katika fani za Sayansi, Teknolojia na nyanja zinazohusiana.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa programu hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Endelevu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Leopold Jacob Mwalongo, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa chuo katika kukuza ushiriki wa wanawake kwenye masomo ya sayansi na kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu.
“Programu hii inalenga kupanua fursa za elimu kwa wanawake waliokosa nafasi ya awali ya kusoma masomo ya sayansi. Kupitia mpango huu, tunachangia kujenga jamii jumuishi na kuongeza idadi ya wanawake katika fani za sayansi na teknolojia. Kwa mwaka wa masomo 2025/2026, jumla ya wanawake 247 wamefanikiwa kujiunga na kuanza mafunzo haya,” amesema Dkt. Mwalongo.
Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya programu hii unaendelea kuonesha dhamira ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ya kuendeleza elimu jumuishi na kuimarisha usawa wa kijinsia, huku ukichangia jitihada za kitaifa za kukuza rasilimali watu yenye ujuzi katika sayansi na teknolojia kwa maendeleo endelevu ya taifa.