Sita wanusurika kifo radi ikiteketeza nyumba Tabora

Tabora. Watu sita wa familia moja, wakazi wa kijiji cha Ulamba, kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora, wamenusurika kifo baada ya kupigwa na radi iliyosababishwa na mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo, huku nyumba yao ikiteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo, Februari 7, 2026.

Tukio hilo limesababisha watu hao kupata majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao, huku moto uliotokana na hitilafu ya umeme iliyosababishwa na radi hiyo ukiteketeza baadhi ya mali zilizokuwemo ndani ya nyumba.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wanafamilia hao, Kurwa Yasin, amesema wakati mvua ikiendelea kunyesha walisikia mngurumo mkubwa wa radi uliowatisha na kuwalazimu kutoka nje ya nyumba.

Amesema walipofika nje walishuhudia moto ukiwaka juu ya paa la nyumba yao, huku baadhi ya ndugu zao tayari wakiwa wamepoteza fahamu na kuungua sehemu za miili yao.

“Yaani mngurumo tuliusikia sijawahi kuusikia maishani. Ulitutisha sana. Tulikuwa ndani tukaamua kutoka nje, ndipo tukakuta moto juu ya paa tayari unawaka,” amesema Kurwa.

Naye Dotto Yasin, mwanafamilia mwingine, amesema baada ya mngurumo mkali aliwaona ndugu zake wakianguka ghafla chini na wakipata majeraha ya moto, hali iliyomfanya atambue kuwa radi ilikuwa imepiga nyumba yao.

“Ni tukio la kutisha sana, linasababisha mshtuko mkubwa. Unasikia kishindo kikubwa halafu watu wanaungua,” alisema Dotto.

Kwa upande wake, jirani yao, Ernest Sitma, amesema walipofika eneo la tukio walikuta majeruhi tayari wametolewa nje ya nyumba, huku moto ukiendelea kuteketeza jengo hilo. Alisema walijaribu kuuzima moto bila mafanikio, sambamba na kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi kabla ya kuwakimbiza hospitalini.

“Tulijitahidi kutoa huduma ya kwanza, kisha tukapata usafiri na kuwakimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, ambako wanaendelea na matibabu,” amesema Sitma.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ulamba, Abdallah Kagusi, amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua, huku akiomba Serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia familia hiyo ili iweze kurejea katika maisha ya kawaida haraka.

“Nawaomba wadau na jamii tushirikiane kuwasaidia wenzetu ili kurejesha hali yao ya maisha,” amesema Kagusi.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, Swaumu Kimaro amethibitisha kuwapokea majeruhi sita na kusema wanaendelea kupatiwa matibabu, huku hali zao za kiafya zikiendelea kuimarika.

“Kwa sasa hakuna anayehitaji rufaa. Wote wanaendelea kutibiwa hapa na hali zao zinaimarika kadri muda unavyokwenda,” amesema Swaumu.