Ukosefu wa taa za barabarani wachochea uporaji Tanga

Tanga. Wakazi wa Jiji la Tanga wamelalamikia ukosefu wa taa za barabarani katika baadhi ya mitaa, wakisema hali hiyo imekuwa ikitumiwa na vikundi vya vijana maarufu kama vishandu kujihusisha na uporaji wa mikoba na simu, pamoja na kuwajeruhi wananchi kwa kutumia silaha za jadi.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa nyakati tofauti wiki hii katika Kata ya Majengo jijini Tanga umebaini mitaa kadhaa haina taa za barabarani, hali inayosababisha kiza kinene nyakati za usiku na kutajwa kuwa kichocheo kikubwa cha vitendo vya uhalifu.

Akizungumza kuhusu changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Anisa, Kata ya Majengo, Halima Mjumbe amesema ukosefu wa taa za barabarani katika mitaa mingi unawapa mwanya wahalifu kutekeleza vitendo vyao.

“Zamani kulikuwa na taa kwenye baadhi ya njia na zilisaidia sana kuimarisha ulinzi. Baada ya taa hizo kuharibika, tumeishi gizani na uhalifu umeongezeka. Maeneo kama Chuda Masiwani yanahitaji sana taa za barabarani,” alisema Mjumbe.

Aliongeza kuwa barabara ya 12 kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga inahitaji kuongezewa taa, huku barabara ya 15 ikiwa haina kabisa taa, isipokuwa barabara kubwa ya Taifa Road.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Fadila, Daima Thabiti, alisema mtaa wake unakabiliwa na vitendo vya ukwapuaji wa simu na mikoba, hasa katika maeneo yenye giza.

“Ukiona watu watatu au wanne wamepanda pikipiki, kuwa makini. Wakikukuta umezembea, wanakupora simu au mkoba, na ukijaribu kupambana unaweza kujeruhiwa, kisha wanatoweka gizani,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Chuda, Rehema Rubinga, alisema kukabiliana na vishandu kutakuwa rahisi zaidi endapo Halmashauri ya Jiji la Tanga itasimika taa za barabarani katika maeneo yanayoripotiwa mara kwa mara vitendo vya uporaji.

“Tunahitaji taa kuanzia Kanisa la Kana hadi Nyinda, maeneo ambayo yana rekodi ya matukio mengi ya uporaji kuanzia saa kumi na mbili jioni,” amesema.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa wa Kata ya Majengo amesema angetamani kuona taa zikifungwa haraka ili kulinda usalama wa watu na mali zao, akieleza kuwa hapo awali taa zilikuwepo lakini ziliondolewa bila maelezo.

“Tunaomba halmashauri kuliweka jambo hili kama kipaumbele. Vijana wengi siku hizi wanataka fedha bila jasho, hivyo mazingira ya giza yanawachochea,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya jitihada za Jeshi la Polisi, taa za barabarani ni muhimu kwani polisi hawawezi kuwepo kila mahali, hivyo jamii inahitaji kushirikishwa katika kuimarisha usalama.

Akizungumzia mpango wa halmashauri, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Juma Hamsini, amesema zaidi ya Sh400 milioni zitatumika kununua taa 200 za barabarani zitakazofungwa katika maeneo korofi.

“Tayari tumeitoa tenda ya ununuzi wa taa 200. Tunatarajia ndani ya wiki moja taa hizo zitawasili na kuanza kufungwa ili kuimarisha usalama wa usiku,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amesema ukosefu wa taa ni kichocheo cha uhalifu; amesisitiza taa zifungwe katika maeneo yenye matukio ya kihalifu na kata zote zilizoathiriwa kuanzisha ulinzi shirikishi.

“Hali imeanza kutulia baada ya kuchukua hatua, lakini ulinzi shirikishi ni muhimu. Kata sita tayari zimeanza, na tunatarajia nyingine zifuate,” amesema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesema limefanikiwa kuwakamata vijana wanaohusishwa na uporaji wa simu na kuwajeruhi wananchi.

Pia, jumla ya simu 60 zimekamatwa; kati ya hizo, 35 zimetambuliwa na kurejeshwa kwa wamiliki wao, huku 25 zikiendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya taratibu za kisheria.