Unguja. Wavuvi na wajasiriamali wa mazao ya baharini wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya Fungurefu na Mkokotoni mkoani Kaskazini Unguja, wameiomba Serikali kuwapa kipaumbele pindi miradi ya masoko ya samaki inayojengwa katika maeneo hayo itakapokamilika.
Ombi hilo limetolewa leo Februari 7, 2026 mbele ya Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mboja Ramadhan Mshenga, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumiaji wa maeneo husika.
Mmoja wa wavuvi hao, Hussein Haji amesema wanayo imani kubwa na Serikali katika kuwaletea maendeleo, lakini wameeleza hofu ya kukosa nafasi ya kuendelea na shughuli zao katika majengo mapya baada ya ujenzi kukamilika na nafasi hizo kutolewa kwa watu wengine.
“Sisi ndiyo tumekuwa tukitumia maeneo haya muda wote. Sasa mazingira yanapoboreshwa, hofu yetu ni kukosa nafasi na kuona majengo mapya yakitolewa kwa watu wengine,” amesema Hussein.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Khamis Ramadhan ambaye amesema uzoefu unaonesha mara nyingi maeneo yanapoboreshwa, watu wapya hujitokeza na wenyeji waliokuwepo awali kusahaulika.
Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Mboja amewatoa hofu wavuvi, waanika dagaa na wajasiriamali wote waliopo katika maeneo hayo, akisema Serikali itahakikisha inawapa kipaumbele waliokuwepo kabla ya kuwahusisha wengine.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imeandaa mipango mikubwa ya ujenzi wa masoko hayo ili kuwaweka wavuvi katika mazingira bora ya kufanyia kazi, kuinua kipato chao na kuboresha maslahi yao.
“Serikali inawajali na kuwazingatia. Ndiyo maana miradi hii imeanzishwa, ili muweze kufanya kazi zenu katika mazingira salama na ya kisasa,” amesema Mboja.
Hata hivyo, amewataka wavuvi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa wizara hiyo wakati ujenzi ukiendelea ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Maeneo ya Kama na Fungurefu yaliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ni maarufu kwa shughuli za uvuvi na uanikaji wa dagaa, ambapo Serikali imeweka mipango ya kusaidia kuboresha shughuli hizo kwa njia za kisasa.
Katika hatua nyingine, wavuvi hao wameeleza changamoto ya kuwepo kwa mwamba wa baharini katika maeneo hayo unaohatarisha usalama wa vyombo vyao vya uvuvi, hivyo kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuuondoa ili waweze kufanya shughuli zao kwa usalama zaidi.
Akizungumzia changamoto hiyo, Naibu Waziri Mboja amesema Serikali inalifanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu ili kuepusha hasara kwa wavuvi, ikiwemo kuvunjika kwa vyombo vyao vya uvuvi.