WITO WATOLEWA, JITIHADA ZA PAMOJA UDHIBITI WA SILAHA HARAMU NCHINI

*********

Kamati ya udhibiti na usimamizi wa silaha  imetakiwa kujikita katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya silaha haramu ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya silaha haramu.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa ufungaji wa kikao cha kwanza cha mafunzo cha kamati ya udhibiti na usimamizi wa silaha, kilichofanyika kwa siku tatu Jijini Dar Es Salaam, wajumbe wakikubaliana kuwa ikiwa elimu itatolewa na jamii ikaelewa madhara ya kusambaa kwa silaha haramu, nchi itakuwa salama.

Mapema akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, IGP Camillus Wambura amesema wajumbe wa kamati hiyo ni watu makini na wameonesha kuwa watakuwa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu yao kutokana na kuwa wabobezi katika nyanja tofauti kutoka Serikalini na sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini na Mrajisi Mkuu wa Silaha DCI Ramadhan Kingai alisema wataendelea kuchukua hatua kali kwa wamiliki wa silaha ambao wamekuwa wakikiuka taratibu za umiliki wa silaha.

Madhara ya kuzagaa kwa silaha haramu kulingana na wajumbe wa Kikao hicho ni pamoja na kutumika katika uporaji wa mali, uporaji wa mifugo, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, kusababisha vifo, majeruhi na jamii kuishi kwa hofu jambo litakalo wasababisha washindwe kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za kujipatia riziki za kila siku hivyo kuathiri maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.