IKICHEZA ugenini kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Yanga imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa AS FAR Rabat katika mechi ya tano ya kundi B kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kipigo hicho kimeifanya Yanga kubaki na pointi tano ikishuka hadi nafasi ya tatu, huku AS FAR Rabat ikipanda nafasi ya pili ikifikisha pointi nane, huku mechi za mwisho zikishikilia hatma ya wawili hao mmoja kufuzu robo fainali.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 7, 2026, bao lililoizamisha Yanga limefungwa na Anas Bach dakika ya 85 kufuati walinzi wa Yanga kujichaganya katika kuokoa hatari na mpira kumkuta mfungaji aliyeachia shuti ndani ya boksi na kipa Djigui Diarra kushindwa kuzuia shambulizi hilo.
Prince Dube aliikosesha Yanga nafasi ya kupata mabao kufuatia nafasi mbili alizopata akiwa katika boksi la mpinzani kushindwa kuzitumia vizuri.
Dube ambaye aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Laurindo Depu, alishindwa kuitumia vizuri nafasi aliyopata dakika ya 76 baada ya kupokea pasi ya Mudathir Yahya, lakini shuti la kwanza alilopiga liligonga nguzo na kurudi, kisha akaunganisha tena, kipa akadaka.
Dakika ya 89, akapokea pasi nyingine ya chinichini ikiwa ni krosi iliyopigwa na Israel Mwenda, akiwa ndani ya boksi akapaisha.
Katika mechi hiyo, Clement Mzize alifanikiwa kucheza kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne tangu alipoumia Septemba 2025 wakati Yanga ikiichapa Wiliete 3-0, hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alimpa nafasi Mzize ya kucheza kuanzia dakika ya 81, akichukua nafasi ya Pacome Zouzoua.
Matokeo hayo yanafanya kutokuwa na mbabe kati ya Yanga na AS FAR Rabat kwani kila mmoja ameshinda kwake bao 1-0, hivyo ikitokea hatua ya makundi imemalizika na timu hizo kulingana pointi, AS FAR Rabat inaweza kuwa juu ya Yanga kwa tofauti ya mabao kwa ujumla.
Kanuni za CAF zinasema hivi: “Hatua ya makundi, timu hupangwa kulingana na pointi (pointi 3 kwa ushindi, pointi 1 kwa sare, pointi 0 kwa kipigo).
“Endapo timu zitafungana kwa pointi, vigezo vifuatavyo hutumika kwa mpangilio huu (Kanuni III. 20 & 21): (i) Pointi zilizopatikana kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana; (ii) Tofauti ya mabao (goal difference) kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolinga[1]na; (iii) Mabao yaliyofungwa kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana; (iv) Mabao ya ugenini yaliyofungwa kwenye miche[1]zo waliyokutana kati ya timu zinazolingana.”
Kanuni imeendelea kufafanua kwamba: “(v) Endapo timu zaidi ya mbili zimelingana, na baada ya kutumia vigezo vyote vya ana kwa ana bado kuna timu zinaendelea kulingana, vigezo vyote vya timu zilizokutana vilivyo juu vitatu[1]mika tena mahsusi kwa kundi hilo dogo la timu zinazolingana; (vi), Tofauti ya mabao katika michezo yote ya kundi; (vii) Mabao yaliyofung[1]wa katika michezo yote ya kundi; (viii) Mabao ya ugenini yaliyofungwa katika michezo yote ya kundi; (ix) Kupigwa kura (drawing of lots).”
Kutokana na hilo, Yanga italazimika mechi ya mwisho nyumbani kuifunga JS Kabylie kwa idadi kubwa ya mabao ili kuweka tofauti ya mabao iwe nzuri kutoka sasa kuwa -2 kufuatia kufunga mawili na kuruhusu manne, wakati AS FAR Rabat ikiwa na +1, imefunga matatu na kuruhusu mawili.
Wakati Yanga ikiikaribisha JS Kabylie, AS FAR Rabat itaifuata Al Ahly ambayo yenyewe unaweza kusema imeshafuzu robo fainali kutokana na sasa kuongoza kundi ikiwa na pointi tisa ambazo timu inayoshika nafasi ya tatu haiwezi kuzifikia.
Yanga inachoomba sasa ni Al Ahly iifunge AS FAR Rabat mechi hiyo ya mwisho, ili isiongeze pointi yoyote kwani zikitoka sare itazima ndoto za Wanajangwani hao kufuzu robo fainali hata wakiichapa JS Kabylie. Katika maombi hayo, Yanga pia iichakaze JS Kabylie kwa kipigo cha mabao kuanzia 3-0 kuweka tofauti yao ya mabao iwe nzuri kulinganisha na AS FAR Rabat ambayo hata ikichapwa 1-0, itakuwa na 0, wakati Yanga ikiwa na +1.