Manyara. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu, John Gwandu, amesema mitandao ya kijamii imekuwa uwanja wa matusi, fujo na mipasho, hali inayochochea chuki na kuharibu misingi ya amani na mshikamano wa Taifa.
Askofu Gwandu amesema licha ya Watanzania kupenda amani, wanachokihitaji zaidi kutoka kwa viongozi wao ni kutendewa haki, kuambiwa neno la matumaini, faraja na la kuponya majeraha yao, badala ya kauli zinazoongeza mgawanyiko.
Amesema mipasho na lugha chafu inayoendelea kushamiri kwenye mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha chuki, huku viongozi wa dini, Serikali na taasisi mbalimbali wakitukanwa waziwazi, hali inayodhoofisha maadili ya jamii.
Askofu Gwandu ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Februari 8, 2026, wakati wa ibada ya kumweka wakfu kuongoza Dayosisi ya Mbulu pamoja na Msaidizi wake, Mchungaji Ezekiel Diyame, iliyofanyika katika Usharika wa Haydom. Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa.
Kauli ya Askofu huyo imekuja katika kipindi ambacho mjadala wa matumizi ya lugha kwenye mitandao ya kijamii umechukua sura pana, ikiwa ni takribani wiki moja tangu Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alipoonyesha wasiwasi kuhusu tabia ya baadhi ya vijana kujibizana na kuwakejeli wazee, akisema vitendo hivyo vinavunja heshima na ni hatari kwa maadili ya jamii.
Akizungumza baada ya kuwekwa wakfu, Askofu Gwandu aliwapa pole Watanzania waliopoteza wapendwa wao wakati na baada ya Oktoba 29, 2025, akitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kulinda amani na mshikamano wa Taifa.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa,akimwingiza kazini Askofu wa Dayosisi ya Mbulu,John Gwandu,leo Jumapili Februari 8,2026 katika Usharika wa Haydom,mkoani Manyara.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa nchi yenye rasilimali nyingi, ikiwemo madini ya Tanzanite na wanyamapori wanaovutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku Watanzania wakijengwa katika misingi ya kupendana, kuheshimiana na kuishi pamoja bila kujali tofauti za dini na makabila.
“Leo misingi hii tuliyojengewa na waasisi wetu imeanza kutoweka. Mitandao ya kijamii, ambayo ni chombo kikuu cha kupashana habari, imegeuka kuwa uwanja wa matusi, fujo na mipasho,” amesema.
Ameeleza kuwa vikundi mbalimbali vimeibuka vikishambuliana, vingine vikitetea upande mmoja na vingine upande mwingine, hali inayopanda mbegu ya chuki ndani ya mioyo ya watu.
Askofu Gwandu amesema kupishana kwa mawazo si jambo baya, akifananisha na tofauti zinazoweza kutokea ndani ya familia, lakini akasisitiza kuwa tofauti hizo zinapaswa kushughulikiwa kwa hekima na mazungumzo.
Amesisitiza kuwa viongozi wa dini, Serikali na vyama vya siasa, kwa kuwa wanasikilizwa na jamii, wana wajibu mkubwa wa kuondoa chuki na kupanda mbegu za upendo, haki, unyenyekevu na matumaini kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo amesema, Serikali inatambua mchango wa kanisa katika kulijenga Taifa kiroho, kimaadili na kijamii, na itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kukabiliana na changamoto za kijamii.
Amesema wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo ubakaji, ulawiti na ndoa za utotoni, akitoa wito kwa kanisa kushirikiana na Serikali katika kukemea vitendo hivyo.
Naye Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa, amesema makanisa yote yanapaswa kuonyesha matokeo chanya kwa kubadili maisha ya waumini, ikiwemo kukemea dhambi bila woga, huku akionya dhidi ya makundi ndani ya kanisa yanayopunguza nguvu ya neno la Mungu.