EKI wa Simba, Antony Mligo amemtaja beki wa kati wa timu hiyo, Rushine De Reuck licha ya ubora alionao kiwanjani, pia ni mchezaji kiongozi ambaye anachukia kufungwa na anapenda wachezaji wenzake wawe bora kiwanjani.
Mligo amejiunga Simba kuziba pengo la Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akitokea Namungo FC, amesema licha ya timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri kwa mechi za karibuni haiondoi ubora wa Rushine.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mligo alisema kwa mabeki wa kigeni ambao amepata nafasi ya kufanya nao kazi anamkubali Rushine kwa sababu ni beki bora na kiongozi uwanjani, uwepo wake Simba unaweza kuwa darasa kwa nyota wengi wanaokubali kujifunza.
“Namkubali sana Rushine, kwa sababu ni beki bora sana na huwa anapenda na wengine wafanye vizuri, ni kiongozi mzuri akiwa uwanjani huwa hapendi kufungwa, kiufupi ni mshindani sana.
“Wachezaji wa aina kama yake ni wachache sana kwa sababu kila mmoja anajipambania yeye, lakini kwa upande wake ni tofauti ni kipngozi uwanjani anapenda kujitoa lakini pia ni mwalimu mzuri wa kuelekeza mazuri kwa wengine.”
Mligo alisema anafurahi kufanya kazi sambamba na beki huyo, anaamini kuna mengi mazuri anayaongeza na kuendelea kuchukua kutoka kwake kwani yeye bado anaendelea kujifunza.
Akizungumzia ligi kwa ujumla, Mligo alisema ni ngumu na wao kama wachezaji wana kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kuirudisha timu hiyo kwenye ushindani na hatimaye kutwaa mataji.
“Ugumu wa Ligi hauondoi sisi kuwa timu bora na shindani kila kitu kinawezekana kutokana na mipango iliyopo hatujawa na muendelezo mzuri hili linatuumiza sisi kama wachezaji na tupo tayari kuipambania timu iweze kufikia malengo,” alisema.