Bima ya afya kwa wote: Mafanikio ya awali, maswali na hatima ya haki ya afya Tanzania

Dar es Salaam. Ndani ya siku 100 za utekelezaji wa awamu mpya ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali iliweka msisitizo mkubwa kwenye ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance – UHI) kama nguzo ya haki ya kijamii na ustawi wa wananchi.

Msisitizo huo ulitolewa Alhamisi, Agosti 28, 2025 na Rais Samia, wakati huo akiwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Aliahidi katika kipindi cha siku 100 ataanza utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote, hatua itakayoanza kwa awamu ya majaribio.

Samia alitoa ahadi hiyo, wakati akizindua rasmi kampeni za CCM za Uchaguzi Mkuu 2025, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam.

Mpango huu ulipokelewa kwa matumaini makubwa, lakini pia uliibua maswali mazito kuhusu utekelezaji wake halisi, uwezo wa mifumo ya afya, na kama kweli inalenga kumlinda mwananchi wa kawaida au kuiongezea mzigo mifumo dhaifu iliyopo.

Kwa miongo kadhaa, huduma za afya nchini zilikuwa zikitegemea kwa kiasi kikubwa malipo ya moja kwa moja kutoka kwa wagonjwa  hali iliyosababisha kaya nyingi kuingia kwenye umaskini au kuchelewesha matibabu kwa kukosa fedha.

Bima ya afya kwa wote inalenga kuvunja mzunguko huo kwa kuhakikisha gharama za matibabu hazibebwi tena na mgonjwa wakati wa dharura, bali zinagawanywa kupitia mfumo wa bima.

Siku 99 tangu kuapishwa kwake, Novemba 3, 2025 uongozi wa Rais Samia umeonyesha msingi wa sera na dira ya kisiasa.

Moja ya mafanikio makubwa ya awali ni kuweka msingi wa kisheria na kisera wa bima ya afya kuwa ya lazima kwa Watanzania wote, huku Serikali ikichukua jukumu la kulipia makundi maalumu yakiwemo wazee, watoto, wajawazito, watu wenye ulemavu na kaya maskini.

Hatua hii inaashiria mabadiliko ya fikra kutoka afya kama huduma ya hiari kwenda afya kama haki ya msingi.

Aidha, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa afya na kupanua wigo wa vituo vinavyokubali bima, jambo linalolenga kuimarisha uwezo wa mfumo kukidhi mahitaji yanayoongezeka kadri wanachama wa bima wanavyoongezeka.

Kwa upande wa sera, UHI imejipambanua kama nyenzo ya utekelezaji wa ajenda pana ya maendeleo ya binadamu na ustahimilivu wa jamii.

Januari 23, 2025 Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act, 2023) alitangaza kuanza rasmi kutumika kwa kitita cha mafao ya huduma muhimu za afya gharama za uchangiaji kwa kitita hicho.

Kitita cha mafao ya huduma muhimu za afya kitagharimu Shi150,000 kwa kaya ya watu sita kwa mwaka.

“Tunaposema kitita cha mafao ya huduma muhimu, tunazungumzia msingi wa ulinzi, ili huduma za lazima zisigeuke mzigo wa kuangusha familia. Bima ni mkataba wa tumaini, unalipa kabla ya dhoruba, ili dhoruba isikivunje,” alisema Mchengerwa.

Kuanza kutumika kwa kitita cha mafao ya huduma muhimu za afya ni hatua ya kihistoria kwani asilimia kubwa ya watakaojiunga awamu hii ya kwanza ambao wanalipiwa na serikali, hawajawahi kuwa katika mfumo wa bima.

Mbali na kifurushi hicho cha msingi, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), utakaosimamia mpango huo, umeandaa vifurushi vingine kulingana na uwezo wa mwanachama ambavyo vitakuja awamu ya pili ya utekelezaji na kuendelea.

Kifurushi cha Tarangire kwa kaya ya watu sita ni Sh796,560; Ngorongoro Sh1,684,800; Mikumi Sh2,621,760; Serengeti Sh3,880,800, huku kifurushi cha juu zaidi cha Tanzanite kikigharimu Sh11,162,640 kwa kaya ya watu sita.

Pamoja na mafanikio ya mwanzo, changamoto kubwa ipo kwenye utekelezaji wa vitendo. Kwanza, uelewa wa wananchi kuhusu bima ya afya kwa wote bado ni mdogo, hasa vijijini.

“Kwa baadhi ya wananchi, dhana ya ‘bima ya lazima’ inaonekana kama kodi mpya badala ya uwekezaji wa afya,” alisema Abdalah Kajula (58) mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wananchi walisema, ubora wa huduma katika vituo vingi vya afya bado haujalingana na matarajio ya wanachama wa bima.

“Upungufu wa dawa, vifaa tiba na watumishi unaweza kuhatarisha imani ya wananchi kwenye mfumo. Endapo mwananchi atalipa bima, lakini akakosa dawa au kuhudumiwa kwa kuchelewa, imani hiyo inaweza kuyumba mapema,” alisema Sesilia Cheso mkazi wa Mbeya ametoa angalizo.

Hata hivyo baadhi yao wamekuwa na maswali kuhusu uwezo wa kifedha wa mfuko wa bima kulipa madai ya vituo kwa wakati.

Wakisema ucheleweshaji wa malipo unaweza kusababisha vituo binafsi au vya imani kusita kupokea wanachama wa bima, jambo linaloweza kupunguza upatikanaji wa huduma.

Hapa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka ameeleza kuwa wameanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na mifumo yote imewekwa sawia ikiwemo kulipa vituo kabla ya kutoa huduma.

Amesema akaunti maalum ya Bima ya Afya kwa Wote tayari imefunguliwa na ipo Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kulipa madai, huku mifumo ya ufuatiliaji ikitumia alama za vidole au utambuzi wa sura (facial recognition).

“Vituo vitatumia alama za vidole na utambuzi wa sura kwa ambao alama zao za vidole zitaonekana kufutika watatumia alama za sura kwenye utambuzi,” amefafanua.

Amesema katika utoaji wa huduma watakuwa wakifanya tathmini na ufuatiliaji kila mwezi kujua nani alitibiwa na magonjwa yapi kwa kuangalia kituo kimetibu idadi ipi na kilitumia kiasi gani katika fungu walilopewa.

“Tutafuatilia karibu, wakisema tumemlaza mgonjwa kwa siku 10 tutaenda kuangalia kama ni kweli kupitia alama za vidole na sura tutafuatilia na kufanya tathmini.”

Aidha amesema kwa wananchi wenye malalamiko watawasiliana kupitia namba ya dharura 199 au kituo cha huduma kwa wateja 0800 787 800, huku maofisa wa NHIF wakiwepo vituoni kusaidia wanachama papo hapo.

Hata hivyo Mchengerwa ameendelea kusisitiza akitoa onyo kwa NHIF na watoa huduma dhidi ya wizi, ulaghai na ubadhirifu wa fedha za bima ya afya kwa wote.

“Sitakubali chini ya uongozi wangu NHIF ichezewe, kwenye hili niko tayari kuchukiwa na watu, ulaghai ukiachwa fedha zinaanza kutoka na kupotea, wahudumu wasiwafanye wananchi wakaikatia tamaa bima na wagonjwa wanarudi kwenye hofu ya gharama mwisho imani ya wananchi itaondoka,” amesisitiza na kuongeza.

“Hata sera itakua ngumu kutekelezeka, ulaghai si wizi wa fedha pekee ni wizi wa huduma, msimamo wa serikali tutalinda mifumo na kulinda wanaofichua maovu. Tutaongeza nguvu kwenye malipo ya madai, tutakagua nyayo za miamala ili kudhibiti na tutagundua mapema kwa ukaguzi wa ndani, tukishirikiana na vyombo vya uchunguzi,” amesema Mchengerwa.

Utekelezaji wa bima ya afya kwa wote si kwa sekta na hospitali za umma pekee, bali ni pamoja na sekta binafsi na hapa Chama cha Watoa Huduma Binafsi wa Afya (APFTHA) wameeleza.

“Upande wetu sisi bado hatujakaa na Wizara ya Afya, tunatarajia kukutana wiki hii. Baada ya kikao nao tutakuwa na majibu mazuri,” amesema Ofisa Mtendaji Mkuu wa APHTHA, Dk Samwel Ogillo.

Tutafanikisha usawa wa afya?

Wataalamu wa afya wamesema kwa mtazamo wa sera, bima ya afya kwa wote ni hatua sahihi kuelekea usawa wa afya. Hata hivyo, mafanikio yake hayataamuliwa na sheria pekee bali na uwekezaji sambamba kwenye miundombinu, rasilimali watu na uwajibikaji.

Hata hivyo wamesema bila kuimarisha zahanati na vituo vya afya vya msingi, hasa vijijini, bima ya afya inaweza kuongeza mahitaji bila kuongeza uwezo wa mfumo kuyakidhi.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema bima ya afya kwa wote si suluhisho la papo kwa changamoto zote za afya, bali ni mwanzo wa safari ndefu ya kujenga mfumo wa afya unaojali utu na haki ya mwananchi.

“Ndani ya siku 100, Serikali imeonyesha dhamira ya kisiasa, kilichobaki sasa ni kuhakikisha dhamira hiyo inageuka kuwa huduma halisi, bora na yenye usawa kwa kila Mtanzania,” amesema Dk Nkoronko.