Challe alia ufinyu wa kikosi KenGold

KOCHA Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe, amesema sababu ya timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri hadi sasa, ni kutokana na ufinyu wa kikosi kilichopo, kwa sababu wachezaji wengi wanacheza maeneo ya ushambuliaji zaidi kuliko eneo la kujilinda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Challe, amesema katika wachezaji wanaocheza nafasi za ushambuliaji ni wengi katika timu hiyo, jambo linalochangia kukosa balansi nzuri msimu huu na kusababisha kuandamwa na matokeo ya kusuasua tangu msimu umeanza.

“Shida kubwa ilianza tulipofungiwa kutofanya usajili wowote kutokana na baadhi ya wachezaji walioondoka kudai stahiki zao, hali hiyo imesababisha kuwabadilisha nafasi baadhi yao uwanjani, ili tu tuendane na mahitaji yetu,” amesema Challe.

Kocha huyo amesema hali hiyo imechangia kurudisha nyuma maendeleo ya kikosi hicho msimu huu, ingawa anaendelea kupambana kwa mechi zilizobakia, hususani kutengeneza balansi nzuri kwenye eneo la kujilinda ambalo ndilo limekuwa ni changamoto.

KenGold iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, ikitokea Ligi Kuu hadi Championship baada ya kuburuza mkiani na pointi 16, msimu huu imeshinda mechi tano, sare tano na kupoteza saba, ikifunga mabao 17 na kuruhusu 18, ikiwa ya tisa na pointi 20.