Conte afichua siri za Yanga

YANGA imejiweka katika hesabu ngumu za kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Kundi B baada ya juzi usiku kufungwa kwa bao 1-0 na As Far Rabat ya Morocco, lakini kiungo wa zamani wa timu hiyo, Moussa Balla Conte amefichua siri za maisha ya muda mfupi ndani ya klabu hiyo.

Conte alisajiliwa kwa mbwembwe kupitia dirisha kubwa la msimu huu akitokea CS Sfaxien ya Tunisia, lakini alishindwa kuwika na kutolewa kwa mkopo kwenda Raja Casablanca ya Morocco inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids na mwenyewe amezungumza na Mwanaspoti na kufichua kilichomkwamisha Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Morocco, Conte amesema amefurahi sana kuungana na kocha Fadlu ambapo kwake ni kama ndoto iliyotimia.

Kiungo mkabaji huyo amesema, Fadlu alionyesha nia ya dhati ya kutaka kufanya naye kazi alipokuwa akiinoa Simba, lakini kilichomkwamisha ni timu aliyokuwa akiifundisha wakati huo kabla ya kutua Raja.

“Nimefurahi kuona kocha Fadlu akiwa na imani na mimi hata baada ya kutoka Simba, kweli kabisa ni mwalimu mzuri ambaye ana jicho la kuona kipaji cha mchezaji mkubwa.

“Baada ya kutua Raja, furaha yangu kubwa ni kuungana na kocha Fadlu ili sasa tuanze kufanya naye kazi kwa nguvu na juhudi zote,” amesema Conte na kuongeza; “Raja ni timu kubwa yenye mashabiki wengi na ninataka kubadilisha heshima yangu kwa kurudisha ubora ule niliokuwa nao ndani ya muda nitakaokuwa hapa.”

Conte amesema, tatizo kubwa kushindwa kuwika akiwa Yanga sio kwamba imetokana na kushindwa kucheza bali hakupata muda wa kuaminiwa kuonyesha uwezo wake.

“Hapa mwishoni nilipata nafasi na watu waliona ubora wangu kwa muda mfupi ila naamini Raja itamrudisha Conte yule ninayemjua mimi,” amesema kiungo huyo raia wa Guinea aliyeongeza; “Tatizo kubwa Yanga halikuwa mimi na wala sijioni kama nilifeli kwa sababu sikupata nafasi ya kucheza muda mrefu na sikuaminiwa ili nionyeshe uwezo wangu.”

Conte alitua Yanga msimu huu akitokea CS Sfaxien ya Tunisia ambako amecheza kwa takribani miezi sita akiwa amesaini mkataba wa miaka mitatu, kisha ametolewa kwa mkopo.

Kabla ya kutua Yanga, tetesi nyingi zilisema kwamba Simba pia ilikuwa mbioni kumsajili Conte na Celestine Ecua ambao wote walitua Jangwani na kucheza kipindi kifupi bila mafanikio na safari yao kuishia kutolewa kwa mkopo, Ecua akitua JS Kabylie.