GF Trucks kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje

Kibaha. Licha ya sheria za nchi kutolazimisha sekta ya viwanda na usafirishaji kutekeleza mipango ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kampuni ya GF Trucks imechukua jukumu hilo kwa hiari kwa kuwekeza katika uhamishaji wa ujuzi na utoaji wa ajira kwa vijana wazawa, hatua inayochangia moja kwa moja maendeleo ya jamii na uchumi wa ndani.

Kwa mujibu wa sheria, ni sekta za madini na mafuta pekee zinazolazimishwa kisheria kutekeleza mipango ya CSR kupitia Sheria ya Madini ya 2010 na Sheria ya Mafuta ya 2015, ambazo zinawataka wenye leseni kuandaa na kutekeleza mipango hiyo kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa. Katika sekta nyingine kama viwanda, usafirishaji, kilimo, benki, bima na mawasiliano, utekelezaji wa CSR hufanywa kwa hiari wa wawekezaji.

Katika mazingira hayo, GF Trucks imejidhihirisha kama mfano wa kuigwa kwa sekta binafsi kwa kuchagua kuwekeza rasilimali zake katika jamii inayozunguka kiwanda chake kupitia kutoa mafunzo ya ufundi, uhamishaji wa ujuzi wa uzalishaji wa viwandani na ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Akizungumza jana Jumamosi Februari 7, 2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 19 ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo, Meneja Mkuu wa GF Trucks, Ezra Mereng amesema uamuzi wa kampuni kuwekeza katika watu ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani na kujenga rasilimali watu yenye ujuzi.

“Licha ya kutokuwa na wajibu wa kisheria kufanya CSR, tumeamua kuwekeza kwa Watanzania kwa kuwajengea uwezo wa kitaaluma, kwa sababu tunaamini ujuzi wa ndani ndio msingi wa maendeleo endelevu ya viwanda,” amesema Mereng.

Amesema kwa kipindi cha miaka 19, GF Trucks imefanikiwa kuunganisha na kuzalisha magari ya mizigo na magari ya kubebea magogo hapa nchini, huku zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wake wakiwa ni Watanzania waliopata mafunzo ya ndani na ya vitendo.

“Leo tunazalisha magari makubwa na madogo hapa hapa nchini, na zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wetu ni wazawa. Hawa ni vijana tuliowachukua kutoka vyuo vya ufundi na kuwanoa kwa vitendo hadi kuwa sehemu ya mnyororo wa uzalishaji,” amesema.

Mereng ameongeza kuwa mkakati huo umeisaidia kampuni kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje, kupunguza gharama za uzalishaji na kwa wakati huo huo kuchangia sera ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chapa na Masoko wa GF Group, Salman Karmal amesema mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita yameipa kampuni ujasiri wa kupanua uzalishaji na kuongeza ajira kwa Watanzania.

“Tunaishukuru Serikali kwa sera rafiki za uwekezaji. Hii imetuwezesha sio tu kuongeza uzalishaji bali pia kupanua mchango wetu kwa jamii kupitia ajira na uhamishaji wa ujuzi,” amesema Karmal.

Amesema GF Trucks pia imeendelea kutekeleza mpango wa kurudisha kwa jamii kwa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu na kudhamini timu ya mpira wa miguu ya Nyumbu FC iliyopo jirani na kiwanda hicho.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Efroza Mwizarubi amesema mafunzo na ajira aliyopata GF Trucks yamebadilisha maisha yake na kumpa fursa ya kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa ndani.

“Si ajira tu, bali ni ujuzi nilioupata hapa ambao utanisaidia maisha yangu yote. Najivunia kuwa sehemu ya kiwanda kinachozalisha magari nchini,” amesema.

Amesema uwekezaji wa hiari wa kampuni kama GF Trucks katika jamii ni kielelezo cha namna sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya Taifa hata pale ambapo sheria haijalazimisha.