ALIYEKUWA beki wa kati wa Simba, Mkongomani Henock Inonga Baka, amejiunga na Al-Zawraa SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq, akiungana na mshambuliaji nyota wa zamani wa kikosi hicho raia wa Cameroon, Leonel Ateba, anayecheza Al Shorta.
Beki huyo aliyewahi kuichezea Simba kuanzia Agosti 15, 2021 hadi Juni 25, 2024, akitokea DC Motema Pembe ya DR Congo, amejiunga na Al-Zawraa akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Kuwait SC ya Kuwait tangu Januari 9, 2025.
Awali nyota huyo alihusishwa kujiunga na Singida Black Stars kwa ajili ya kuchukua nafasi ya beki wa kati, Anthony Tra Bi Tra raia wa Ivory Coast, aliyeondoka dirisha dogo la Januari 2026, ili akatafute changamoto sehemu nyingine mpya.
Mbali na kucheza Simba na DC Motema Pembe, Inonga amecheza pia OC Renaissance du Congo ya DR Congo na AS FAR Rabat ya Morocco, ambapo amejiunga na Al-Zawraa inayoshika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya Iraq.
Al-Zawraa inashika nafasi hiyo ya tano na pointi 31, msimu huu baada ya kushinda mechi nane, sare saba na kupoteza mmoja tu kati ya 16, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa pia mara 10.
Baada ya Inonga kukamilisha dili hilo, kwa sasa anaungana na Ateba katika Ligi Kuu ya Iraq, ambapo mshambuliaji huyo wa Cameroon tayari amefunga mabao 10 na kuasisti moja, tangu ajiunge rasmi na kikosi hicho cha Al Shorta, Agosti 24, 2025.
Ateba aliyejiunga na Simba Agosti 15, 2024, akitokea USM Alger ya Algeria, katika kipindi cha mwaka wake mmoja akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi, alihusika na mabao 17 ya Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, baada ya kufunga 13 na kuasisti manne.