DILI la aliyekuwa beki wa kushoto wa KMC, Rahim Shomary kujiunga na FK Zhenys inayoshiriki Ligi Kuu ya Kazakhstan, limeshindwa kukamilika, baada ya nyota huyo kuamua kurejea nchini na kutua Singida Black Stars.
Nyota huyo aliyejiunga na Ghazl El Mahalla ya Misri, Julai 14, 2025 na kusaini mkataba wa miaka mitatu baada ya kuachana na KMC, inaelezwa hakufurahia maisha ya Misri na ndio sababu ya kuomba kupatiwa timu nyingine kwa ajili ya kuitumikia.
Hata hivyo, Singida ilikuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na uongozi wa Ghazl El Mahalla ya Misri inayommiliki kwa sasa, ingawa FK Zhenys inayoshiriki Ligi Kuu ya Kazakhstan iliingilia kati na kuweka ugumu kwa nyota huyo kurejea Tanzania.
Baada ya hapo, Singida ikamsajili beki wa kushoto wa Dodoma Jiji, Miraji Abdallah ‘Zambo’, ili awe mbadala wa Shomary, japo nyota huyo aliomba kwa uongozi wa Ghazl El Mahalla umpe nafasi ya kuamua mwenyewe sehemu anayotaka kwenda kucheza.
Mmoja wa rafiki wa nyota huyo, aliliambia Mwanaspoti baada ya mazungumzo hayo Ghazl El Mahalla ikamruhusu achague sehemu ya kwenda, ndipo mchezaji mwenyewe akaamua kurudi Tanzania, akihofia huenda angekutana na changamoto Kazakhstan.
“Mojawapo ya sababu ya kuondoka Misri ni kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwake na hajapata pia nafasi ya kucheza mara kwa mara, hali hiyo ilisababisha kutokwenda Kazakhstan, akihofia huenda mambo yakajirudia,” kilisema chanzo hicho.
Beki huyo ni miongoni mwa nyota walioonyesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha KMC, huku msimu wa 2023-2024 wa Ligi Kuu Bara, akichaguliwa mchezaji bora chipukizi, akiwashinda Semfuko Charles aliyekuwa Coastal Union na Constantine Malimi aliyekipiga Geita Gold.
Ubora na mwendelezo wa wachezaji hao ukafungua milango ya kuonekana na timu nyingine, ambapo Rahim alipata dili kwenda Misri, huku Semfuko akajiunga na Simba, wakati Malimi kwa sasa anaitumikia Mtibwa Sugar.