Kinachokwamisha wagonjwa wa kifafa kupata matibabu

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kifafa kesho, Februari 9, 2026, imani potofu juu ya ugonjwa huo na unyanyapaa umetajwa kama kikwazo kikuu kwa wagonjwa kutafuta matibabu kwa wataalamu wa afya nchini.

Wataalamu wanaeleza kuwa kifafa huanza baada ya athari kwenye ubongo, na mtu hupata mshituko katika eneo hilo na kusababisha degedege au kuanguka, ukubwa wa mshituko ukitofautiana kulingana na hali ya mgonjwa.

Akizungumza leo, Februari 8, 2026 kwa niaba ya Chama cha Wenye Kifafa Tanzania (TEA), Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu na Upasuaji wa Ubongo, Dk Patience Njenje, amesema kifafa ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa endapo mgonjwa atapata matibabu kikamilifu.

“Zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye kifafa nchini Tanzania huanza kwa kushauriana na waganga wa jadi na viongozi wa kiroho, kutokana na imani kuwa degedege husababishwa na nguvu za kishirikina kama vile mapepo,” amesema Dk Njenje.

Dk Njenje amesema kwamba endapo mgonjwa ataonana mapema na daktari na kupata matibabu, anaweza kuishi maisha yasiyo na tabu.

Akielezea ukubwa wa tatizo hilo nchini, Dk Njenje amesema Tanzania ni moja ya nchi zenye baadhi ya vijiji vyenye idadi kubwa ya walioathirika na kifafa, kufikia watu 37.5 kwa kila watu 1,000, ikiwa na wagonjwa 73 hadi 111 kwa kila 100,000, huku wagonjwa wapya wakiongezeka kila mwaka.

Kwa mujibu wa Dk Njenje, takribani asilimia 60 ya wagonjwa wa kifafa hufika vituoni vya afya baada ya wastani wa mwaka mmoja tangu kupata degedege kwa mara ya kwanza.

Amesema kwamba asilimia tano hadi 10 pekee ndio wanaopata dawa sahihi na ufuatiliaji wa kitaalamu mara kwa mara.

Kutokana na hali hiyo, Dk Njenje amesema pengo la uchunguzi na matibabu bado ni kubwa ingawa kumekuwa na juhudi za kuondoa changamoto hiyo.

“Pengo hilo limepungua kutoka karibu asilimia 100 miaka 60 iliyopita, hadi asilimia 95 miaka 30 iliyopita, na kwa sasa likiwa takribani asilimia 50 katika baadhi ya maeneo,” amesema.

Dk Njenje amesema kuwa kwa familia nyingi, kifafa bado kimezungukwa na hofu na kutoelewana.

“Katika wiki hii, tunafanya shughuli za kuelimisha jamii kuhusu kile kifafa ni, na kuvunja imani potofu na unyanyapaa unaoendelea kuwatenga wagonjwa,” amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Kifafa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu ‘Tushirikiane kwa huduma bora za kifafa Tanzania’, yenye lengo la kuhimiza uboreshaji na upatikanaji mpana wa huduma kwa watu wanaoishi na kifafa.

Daktari huyo amesema katika kaya nyingi, kifafa bado hujadiliwa kwa siri na kwa sauti za chini, huku kipaumbele katika sekta ya afya kikiwa ni magonjwa ya kuambukiza kama VVU/Ukimwi na malaria, na magonjwa yasiyoambukiza kama kifafa yakiachwa nyuma.

Kwa upande wake, James Mollel, mkazi wa Arusha, akisimulia ugonjwa wa kifafa unavyomtesa, amesema maisha yake yamekuwa na changamoto nyingi.

“Nilipoanza kupata degedege, watu wengi waliniogopa na kunitenga, wakidhani nimelogwa. Nilifukuzwa kazi, nilikosa marafiki, na familia ilichelewa kunipeleka hospitali. Nilipata majeraha mara kadhaa kutokana na kuanguka ghafla hadharani.

“Dawa zilichelewa kupatikana na zilikuwa ghali, hali iliyonifanya nikae bila matibabu kwa muda mrefu,” amesema.

Amesema anaendelea kupambana, akitamani jamii ielewe kifafa ni ugonjwa unaotibika na wagonjwa wanahitaji msaada na heshima ili waepuke ubaguzi, woga na dhuluma.

Mollel ameiomba jamii na wadau wa afya waweke kipaumbele elimu, matibabu, na ulinzi wa haki za watu wenye kifafa kote nchini Tanzania.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa takribani asilimia 50 hakuna sababu maalumu ya kifafa, na sababu zinazojulikana zinajumuisha maambukizi, mabadiliko ya mwili, pamoja na uharibifu wa kinga.

Sababu nyingine ni ugonjwa wa kiharusi unaopunguza kiwango cha oksijeni kinachofika kwenye ubongo, maambukizi ya ubongo, na uvimbe kwenye ubongo.

Kifafa ni ugonjwa sugu usioambukiza wa ubongo unaowaathiri watu wa rika zote, takribani watu milioni 50 duniani wanaishi na kifafa, na kuufanya kuwa miongoni mwa magonjwa ya mfumo wa fahamu yanayoongoza kwa wingi duniani.

WHO inaeleza kuwa karibu asilimia 80 ya watu wenye kifafa wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Kulingana na shirika hilo, inakadiriwa kuwa hadi asilimia 70 ya watu wanaoishi na kifafa wanaweza kuishi bila degedege iwapo watagunduliwa mapema na kutibiwa ipasavyo.

Hatari ya kufa mapema kwa watu wenye kifafa ni mara tatu zaidi ikilinganishwa na wengine.

Robo tatu ya watu wenye kifafa wanaoishi katika nchi zenye kipato cha chini hawapati matibabu wanayohitaji.

Kifafa kinachangia kwa kiwango kikubwa mzigo wa magonjwa duniani, kikikadiria kuwaathiri takribani watu milioni 50.

WHO inakadiria uwiano wa watu wenye kifafa hai (yaani wanaoendelea kupata degedege au wanaohitaji matibabu) kuwa kati ya watu 4 hadi 10 kwa kila 1,000.

Kiwango cha dunia, takribani watu milioni 5 hugundulika kuwa na kifafa kila mwaka.

Katika nchi zenye kipato cha juu, inakadiriwa kuwa watu 49 kwa kila 100,000 hugunduliwa na kifafa kila mwaka.

Hata hivyo, katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, kiwango hicho kinaweza kufikia hadi watu 139 kwa kila 100,000.

Kwa mujibu wa WHO, asilimia 80 ya watu wanaoishi na kifafa duniani wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.