BAADA ya kuanza kazi ndani ya kikosi cha Songea United, kiungo mshambuliaji, Shaban Ada amesema hesabu zake ni kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kuimarisha kiwango chake, kuonekana na kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Ada amejiunga na Songea United dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 30, 2026 akitokea Stand United ya Shinyanga inayoshiriki Ligi ya Championship ambayo alikuwa ameifungia mabao mawili na assiti tatu.
Kiungo huyo ni miongoni mwa wachezaji 10 waliolikimbia ‘Chama la Wana’ dirisha dogo, wengine ni Raymond Masota, Amri Msenda, Paschal Wagana, Abel Hegela na kipa John Mwanda.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ada anayemudu pia kucheza kiungo mkabaji akiwa tayari ameshaichezea Songea United mechi moja, alisema klabu hiyo ni sehemu sahihi kwake kwani itamsaidia kuonesha uwezo wake katika soka.
“Nimepata mapokezi mazuri na nimebahatika mechi yangu ya kwanza tu nimeanza, napambana niendelee kupata nafasi ya kucheza mara nyingi ili kuonesha uwezo wangu, wenye macho wakiniona nipate timu nzuri hasa za Ligi Kuu, huo ndiyo mpango wangu,” alisema Ada.
Mchezaji huyo wa zamani wa Lipuli, Geita Gold na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Boys, alisema ushindani uliopo Ligi ya Championship ni fursa nzuri kwa wachezaji kupambana na kujitangaza ili kupanda madaraja na kutimiza ndoto zao za kucheza timu kubwa na soka la kimataifa.
“Nimekuja Songea United kuongeza nguvu kwenye timu, hivyo nitapambana kuhakikisha hapa nilipoikuta timu na kuisogeza mbele zaidi kwani matarajio yangu ni kucheza nje ya nchi,” alisema Ada na kuongeza.
“Lakini nisipobahatika kwenda nje basi nicheze Ligi Kuu hapa nyumbani kwasababu unajua sisi wachezaji ambao hatuna mawakala wakati mwingine ni ngumu kusogea juu tunakuwa hatuna watu wa kutuhangaikia,” alisema kiungo huyo.