KOCHA wa JKT Queens, Kessy Abdallah amesema ushindani wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu ni mkubwa kiasi kwamba kosa dogo linaweza kuigharimu timu kisaikolojia.
Kessy aliyejiunga na JKT msimu huu akitokea African Sports ya Tanga ameanza vibaya msimu huu ukitofautisha na msimu uliopita kwenye mechi tisa ameiongoza JKT kushinda saba, kupoteza moja shisi ya Yanga Princess 1-0 na sare moja.
Kessy amesema ligi ya msimu huu imekuwa tofauti na misimu iliyopita kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na klabu nyingi hali inayoongeza presha kwa wapinzani wao..
Kocha huyo alifafanua, timu inapopoteza mechi moja au mbili, hali hiyo inaweza kuiathiri akili ya mchezaji na kikosi kwa ujumla hasa kwa timu kama JKT inayofuatiliwa na wengi WPL.
“Ushindani ni mkubwa sana, ukiteleza kidogo tu unaanza kupata tabu kiakili kwa sababu wapinzani wako wanaendelea kushinda ukizingatia na malengo yaliyopo mbeleni,” amesema Kessy.
Akizungumzia idadi ndogo ya mechi walizocheza, Kessy amesema sababu kubwa ni wachezaji wengi wa JKT Queens kuitwa kwenye timu za taifa kwa ajili ya majukumu mbalimbali ya kimataifa.
“Tumekuwa na wachezaji wengi walioko kwenye timu za taifa, ndiyo maana baadhi ya mechi zetu zimeahirishwa ni jambo la kujivunia na linaonyesha tuna wachezaji wenye kiwango cha juu kuitwa ngazi zote za taifa.”
Tangu ajiunge na JKT Kessy amechukua ubingwa mara mbili, Ngao ya Jamii mbele ya wapinzani wao Simba wakiifumua mabao 2-1 na ubingwa wa CECAFA.