Dar es Salaam. Katika mabadiliko ya kasi ya maisha ya sasa, wazazi wengi wamejikuta wakilea watoto wao katika mazingira ya mijini yenye shinikizo la kazi, teknolojia na majukumu mengi ya kifamilia.
Katika muktadha huo, dhana ya kuwapeleka watoto kuishi au kumtembelea bibi na babu imeanza kupungua, licha ya kuwa na faida kubwa katika malezi na makuzi ya mtoto.
Wataalamu wa malezi na baadhi ya wazee wanasema uhusiano wa karibu kati ya watoto na wazee wao ni nguzo muhimu katika kujenga maadili, utambulisho na ustawi wa kisaikolojia kwa mtoto.
Mtaalamu wa saikolojia ya watoto, Dk Neema Mwakyusa aliniambia kuwa bibi na babu wanayo nafasi ya kipekee katika maisha ya mtoto, kwa sababu hawana shinikizo kubwa la nidhamu kali kama wazazi.
“Watoto wanapokuwa kwa bibi na babu, hupata upendo wa ziada, uvumilivu na usikivu ambao husaidia kukuza afya ya akili na kujiamini kwao,” aliniambia Dk Mwakyusa.
Nilimuelewa na nikaanza kuchunguza, nikabaini kwamba watoto wengi wanaokulia kwa bibi na babu, huwaona kama ni watu wanaowajali sana na kuwathamini, kuliko baba na mama.
Na wengi hujihisi wako huru kusema na kufanya chochote, na hata akikosea, basi hijikuta wako huru zaidi kujieleza na wakapata suluhisho kuliko kwa wazazi.
Kwa upande wa maadili na utamaduni, bibi na babu huchukuliwa kuwa hazina ya historia na mila za familia.
Mwanahistoria na mhadhiri wa chuo kikuu, Profesa Hamisi Mkwawa anasema watoto wanaoishi karibu na bibi na babu hupata fursa ya kujifunza simulizi za ukoo, mila na desturi ambazo mara nyingi hazipatikani shuleni.
“Kupitia hadithi na maisha halisi ya bibi na babu, mtoto hujifunza heshima, subira, mshikamano na utu, ambayo ni misingi muhimu ya jamii ya Kitanzania,” anasema Profesa Mkwawa.
Mbali na kujifunza maadili, kuwepo kwa watoto kwa bibi na babu pia husaidia kupunguza mzigo kwa wazazi, hususan katika familia ambazo wazazi wote wanafanya kazi.
Hata hivyo, katika familia nyingi za Kiafrika zama hizo, malezi yalikuwa jukumu la familia nzima. Mtoto anapokuwa kwa bibi na babu kwa muda, mzazi alikuwa anapata nafasi ya kupanga majukumu ya kiuchumi na kijamii bila hofu kubwa juu ya usalama wa watoto wake.
Na lilikuwa likifanyika hivyo na babu na bibi walikuwa wakiwasiliana kwa karibu sana na watoto wao wanaowapelekea wajukuu ili kuepusha migongano ya kimalezi.
Faida nyingine inayotajwa ilikuwa ni kukuza mshikamano wa kizazi. Watoto wanapokua, wakijua na kuelewa maisha ya wazee wao, walikuwa wakijifunza kuthamini uzee na kuepuka mitazamo hasi dhidi ya wazee.
Katika muktadha huo, wazazi wa sasa wanapaswa kutambua kwamba watoto wanaolelewa karibu na bibi na babu, hukua wakiwa na heshima na huruma kwa wazee wengine katika jamii.
Na hii inatufundisha kwamba mtoto akimzoea bibi au babu nyumbani, hawezi kumdharau mzee barabarani; humwona kama sehemu ya familia yake.
Hata hivyo, wazazi mnapaswa kuzingatia kuwa, unapoamua kuwapeleka wajukuu kwa bibi na babu, mzingatie hali ya kiafya na uwezo wa wazee hao.
Haitakuwa busara kumwachia mzazi wako majukumu mazito ya kukulelea wanao bila ya kumpatia msaada.
Na wazazi wanapokumbushwa kuwapeleka wajukuu kwa wazazi wao, haimaanishi kwenda kuwatwisha mzigo, bali kujenga ushirikiano wa malezi.
Kwa jumla, kuwapeleka watoto kwa bibi na babu si kosa, bali ni uwekezaji katika malezi jumuishi na endelevu.
Katika dunia yetu hii inayobadilika kwa kasi kubwa, uhusiano wa vizazi tofauti unasaidia watoto kukua wakiwa na mizizi imara ya maadili, utambulisho wa kitamaduni na usalama wa kihisia.
Kwa kufanya hivyo kwa mipango mizuri, familia hujikuta ikinufaika na hupata kizazi chenye misingi imara ya utu na mshikamano.