Dar es Salaam. Umoja wa Madereva wa Malori, Mabasi na IT–Tanzania (Tatamata) umetishia kusitisha shughuli zao nchini, kushinikiza kupatikana kwa kiongozi wao, Godlove Materu, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Wakati madereva hao wakitishia mgomo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekanusha madai ya kutekwa kwa Materu, likithibitisha kuwa linamshikilia kwa uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za kisheria.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 8, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema Materu anashikiliwa kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotokea katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe.
“Tunamshikilia kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma mbalimbali. Si muda mrefu tutatoa taarifa rasmi kwa umma, hasa kutokana na uvumi unaoenea mitandaoni kuwa ametekwa,” amesema Kamanda Senga.
Alipoulizwa kwa nini Jeshi la Polisi halikutoa taarifa mapema kwa umma, Kamanda Senga amesema hatua za kiuchunguzi ndizo zilizosababisha kuchelewa kwa taarifa hiyo.
“Hatua za upelelezi ndizo kipaumbele. Wananchi wawe na amani, yupo mikono salama, na tutatoa taarifa kwa umma kwa wakati,” amesema.
Tatamata kilitangaza mpango wa kusitisha shughuli zake kuanzia Februari 10, 2026 iwapo kiongozi wake hatapatikana, huku kikivitaka vyombo vya ulinzi kuchukua hatua za haraka kumtafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Makamu Mwenyekiti wa Tatamata, Yohana Mwanyaga amesema kiongozi wao aliyekuwa mstari wa mbele kupigania haki za madereva ametekwa, na juhudi zote za kumtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi hazijazaa matunda.
“Tumezunguka vituo vyote vya polisi bila mafanikio. Endapo hatapatikana ndani ya siku mbili zilizobaki, tutasitisha shughuli zetu,” amesema Mwanyaga.
Mwanyaga amesema kiongozi huyo wa Tatamata, alipotea wakati chama hicho kikiwa katika hatua za mwisho za kuwasilisha kero za madereva Wizara ya Kazi, ambapo walikuwa walikuwa wamekubaliana kukutana Februari 16, 2026.
Amesema chama hicho hakiwezi kukubali kiongozi wao kupotea katika mazingira ya kutatanisha, na kusisitiza kuwa shughuli zote zitasitishwa hadi atakapopatikana.
“Kama ana tuhuma zozote, basi afikishwe kwenye vyombo vya sheria badala ya kushikiliwa bila taarifa, huku familia yake ikiendelea kuhangaika kumtafuta,” amesema.
Mwanyaga amesema madereva nchini hawasikilizwi ipasavyo na wameachwa kama watoto yatima, hali inayowaacha wamiliki wa vyombo vya usafiri kufanya wanavyotaka bila udhibiti wa kutosha.
“Mateso yameachwa kwa madereva. Tunaiomba Serikali isimamie kikamilifu sekta ya uchukuzi. Madereva hawathaminiwi, wengi wakiendelea kuishi katika umaskini, huku wanaopigania haki zao wakikumbana na vitisho,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tatamata, Gerald Manyauka amesema chama hicho hakielewi sababu za kutoweka kwa kiongozi wao, na kusisitiza kuwa endapo hatapatikana, shughuli zote zitasimamishwa ili kuhakikisha anapatikana.
Manyauka amesema Tatamata haina mgogoro na vyombo vya dola, Serikali wala wadau wa sekta ya uchukuzi, bali wanawaomba kushirikiana katika juhudi za kumtafuta kiongozi wao.
Naye Wakili wa chama hicho, Aloyce Komba, amesema mbali na kusitisha shughuli, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa kufungua kesi mahakamani.
“Tutaenda mahakamani kutafuta majibu kuhusu alipo kiongozi wetu. Ulinzi wa raia na mali zao ni jukumu la Jeshi la Polisi, hivyo tunaliomba lichukue hatua stahiki,” amesema Komba.
Ameongeza kuwa madereva wengi wameguswa na tukio hilo na wanahisi kuwa wananyanyaswa.
Kwa mujibu wa mke wa Godlove Materu, Martha Mushi, mumewe alipotea tangu Alhamisi, Februari 5,2026 saa tatu asubuhi, katika eneo la Chapwa, Tunduma mkoani Mbeya.
Amesema Materu alikuwa katika kibanda chake cha biashara ya maji na vinywaji baridi, ambacho hakikuwa kimemaliza mwezi mmoja tangu kufunguliwa, walifika watu watatu wakiwa na gari aina ya Land Cruiser jeuoe waliovaa kiraia na wakamkamata bila kujitambulisha, wakafunga kibanda chake kisha wakaondoka naye bila kutoa maelezo yoyote,” amesema Mushi.
Ameeleza baada ya tukio hilo alianza kumtafuta kwa kuripoti vituo mbalimbali vya polisi Tunduma, lakini jina la mumewe halikuonekana miongoni mwa watuhumiwa waliokuwepo.
“Nilikwenda pia Kituo cha Polisi Vwawa bila mafanikio, ndipo nikashauriwa nirudi Tunduma kuandikiwa ripoti. Niliandikiwa RB namba 435/2026 na kuendelea na juhudi za kumtafuta,” amesema.
Amesema tangu siku hiyo familia imeendelea kumtafuta kwa kushirikiana na viongozi wa chama cha madereva, huku wakizunguka maeneo mbalimbali kujua alipo bila mafanikio.