Bwana Yesu apewe sifa mtu wa Mungu, nakusalimu katika Jina la Yesu Kristo aliye hai. Ni imani yangu kuwa Mungu ameendelea kuwa mwaminifu kwako tangu mwaka jana hadi leo hii, kwa hakika hata sasa yeye ni Ebenezer.
Namtuza Bwana kwa ajili ya mwaka 2025 kwani alinipa kibali cha kusema nawe kwa habari ya Ufalme wa Mungu, nitumie nafasi hii kushukuru uongozi wa gazeti la Mwananchi kwa maono haya makubwa ya kuhakikisha roho za watu zinaokolewa Mungu awabariki.
Nikushukuru wewe ambaye kila Jumapili umekuwa ukifuatilia mahubiri haya, Mungu akubariki na akujibu kila hitaji la moyo wako.
Tumepokea shuhuda nyingi mwaka jana, tunaimani mwaka huu pia Mungu atakuhudumia, Bwana Yesu asifiwe!
Leo tumepewa ujumbe unaosema “Unaposaidia mhitaji, unagusa moyo wa Mungu”. Najua kila tunapoanza mwaka, kila mmoja huweka malengo na hujitahidi kadiri anavyoweza ili kuhakikisha kuwa yale aliyoyapanga yanatekelezeka.
Leo nataka nikupe changamoto, Je kwa malengo uliyojiwekea mwaka huu 2026 umejipangaje kuwasaidia wahitaji?
Yakobo:1:27, Neno la Mungu linasema “Dini iliyosafi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao”. Tumekuwa na wahitaji tena walio katika dhiki kweli kweli, wako waliopata msaada na wako ambao bado hawajasaidiwa kabisa, na hawajui kesho yao itakuwaje lakini swali la kujiuliza ni je, tumefanya nini kwa ajili yao?
Lini tumefika kwao na kuwatia moyo au kuwapa neno la faraja na matumaini, kulingana na ugumu wa maisha walionao hata kuwafiki imekuwa ni changamoto. Wachache wao wamesaidiwa kwa sababu ya mahusiano, huenda na wewe yupo unayemsaidia kwa sababu tu unafahamiana naye au unamazoea naye, lakini vipi wale ambao haufahamiani nao? Wapo wahitaji wengi wametuzunguka hebu jiulize mara ya mwisho kufanya jambo kwa ajili yao ilikuwa lini?
Mpendwa, Mungu anapokubariki anatamani nawe uwe baraka kwa wengine. Natamani mwaka huu uwe mfano mahala unapoishi au unapofanyia kazi Mungu akufanye kuwa baraka kwa watu wa nyumbani mwako na wale wanaokuzunguka kwani unapofanya hivyo unagusa moyo wa Mungu, naye hawezi kukuacha.
Kuna msemo usemao “Mkono unaotoa ndiyo unaopokea”, hivyo kwa kadri unavyosaidia wahitaji ndivyo unavyozidi kubarikiwa. Mungu ametubariki kwa viwango tofauti tofauti ndio maana tunasoma kwa habari ya maskini na tajiri katika ile Luka 16:19-21. Tajiri alikuwa na kila kitu lakini ni nini alifanya kwa yule maskini hakuna! Maskini alitamani kujishibisha kwa makombo tena yaliyoanguka katika meza ya tajiri, najiuliza furaha ya Mfalme ilikuwa ni nini, alikuwa naye kila siku lakini hakuweza kufanya jambo kwa ajili yake, ni kweli kwamba hakuwa na namna ya kumsaidia? Hakuwa na chakula cha kumpa? Hakuwa na mavazi? Luka 12: 48b inasema “Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi”. Mungu anapokubariki siyo kwa faida yako peke yako bali ni kwa ajili ya ufalme wake ili jina lake liendelee kutukuzwa kwani sisi tu wafuasi wa Kristo hivyo hatuna budi ketenda kama Kristo.
Mathayo 25: 35-40. Neno la Mungu linasema. “Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha, nalikuwa uchi mkanivika; nalikuwa mgojwa mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni mkanijia”. Kutokana na neno hilo tunaona kuwa, kumbe tunao wengi waliokatika changamoto mbalimbali na wanahitaji msaada ili waweze kutoka katika dhiki waliyo nayo. Kuna baadhi ya watu ambao wanapika chakula kingi hadi wanamwaga, unapokea mgeni unaishia kumwangalia hata maji ya kunywa tu huwezi mpatia ili hali, hali yake unaiona, kuna wageni wanaruhusiwa kukaa sebuleni na wengine tunawapa viti huko huko nje na hawaruhusiwi kuingia ndani, kuna nguo sasa ni mwaka wa kumi bado unayo lisha ya kuwa kila toleo unanunua mpya ila kutoa tu ile ya zamani ni changamoto, tunao wagojwa wameugua muda mrefu hata kufika kumuona na kumtia moyo imekuwa pia vigumu. Lakini ngoja nikwambie mstari wa 40 neno la Mungu linasema “…na Mfalme atajibu, akiwaambia, amini nawaambia kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
Ni maombi yangu kwa msimu huu wa 2026, Mungu akupe neema ya kutambua kuwa yale maombi umeomba, Mungu anapokujibu si kwa ajili yako peke yako bali amekuamini na akaamua kupitisha baraka hizo kwako ili nawe uweze kufanyika baraka kwa wengine.
Wakati mwingine tunasaidia watu wasio sahihi ndio maana hatuwezi kuziona baraka za Bwana. 1Timotheo 5:3. “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli” kumbe wako wajane wasio wajane kwelikweli, hawa wanauwezo wa kujihudumia lakini kwa upande mwingine wako wajane walio wajane kwelikweli hawa tunawajibika nao na kanisa linawajibika nao. Hebu tusaidiane, kanisani kwenu mna utaratibu gani wa kuwasaidia wajane, yatima au wahitaji? Hivi unawafahamu kweli wale wa kanisani kwako au mtaani kwenu? (walio wahitaji kwelikweli).
Mwaka huu unapoomba mafanikio katika yale uyafanyayo hakikisha unagusa Moyo wa Mungu kwa kuwasaidia wahitaji na Mungu atakubariki.