Majeraha yamtibulia Kapera Polisi Tanzania

ALIYEKUWA mshambuliaji wa maafande wa Polisi Tanzania, Ramadhan Kapera, amejiweka kando na kikosi hicho, licha ya hivi karibuni kuanza mazoezi na timu hiyo, baada ya kusumbuliwa na jeraha la goti alilolipata kufuatia kupata ajali ya gari.

Nyota huyo aliyeitumikia timu hiyo msimu wa 2020-2021, alirejea tena ndani ya kikosi hicho msimu huu, baada ya kuachana na TMA FC ya jijini Arusha inayoshiriki pia Ligi ya Championship, ingawa ameachana nayo mwa makubaliano ya pande mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kapera amesema kwa sasa anajisikia vizuri baada ya kuanza mazoezi mepesi kutokana na majeraha ya goti na kifua aliyopata wakati wa ajali iliyotokea, ingawa ameondoka kikosini kutokana na mambo kadhaa yaliyotokea.

“Nisingependa kuweka wazi kilichotokea ila, niseme tu nimeachana na Polisi Tanzania, kwa sasa naendelea na mazoezi yangu binafsi ya utimamu wa mwili, mashabiki zangu waendelee kunisapoti japo hawajaniona uwanjani muda mrefu,” amesema Kapera.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Mbeya Kwanza, Geita Gold, KMC na Ihefu kwa sasa Singida Black Stars, msimu uliopita wa 2024-2025, aliifungia TMA mabao sita ya Ligi ya Championship, japo safari hii mambo yamekuwa ni magumu kwa upande wake.