Mohamed Badru: Shilla atang’aa Sweden

KOCHA wa zamani wa Azam FC, Mohamed Badru amesema anajivunia kuona vijana aliowafundisha kwenye timu za vijana wakipata nafasi kimataifa baada ya Mohamed Shilla kutambulishwa AIK ya Sweden.

Badru aliyemfundisha Shilla alipokuwa Azam FC ya vijana, amesema kiungo mshambuliaji huyo ana nidhamu, akili ya mpira na uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja, vitu vinavyompa nafasi ya kufanya vizuri hata kwenye ushindani wa soka la Ulaya.

“Unapowaona vijana mliowalea wanapata nafasi kama hizi, inakupa furaha kubwa. Shilla ni mchezaji anayesikiliza maelekezo, ana akili ya mpira na anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji au mshambuliaji wa kati ninaamini ana uwezo wa kufanya vyema,” amesema Badru.

“Vijana waliopita mikononi mwangu wamefanikiwa kuanza maisha yao ya mpira, wapo kina Cyprian Kachwele, wengine wapo Ligi ya Zanzibar kwahiyo miaka mitatu niliyokaa nao imekuwa ya mafanikio makubwa.”

Badru aliongeza hatua ya Shilla kwenda Ulaya inapaswa kuwa chachu kwa vijana wengine waliopo kwenye akademi na timu za vijana, akisisitiza kuwa mchakato wa kulea wachezaji ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu na nidhamu.

AIK inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden (Allsvenskan), wiki iliyopita ilimtambulisha rasmi Mohamed Shilla kama mchezaji mpya, baada ya kumpa mkataba wa miaka minne utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2030.

Shilla ataaanzia kuitumikia AIK katika timu za vijana huku benchi la ufundi likiendelea kumfuatilia kwa karibu ili kutathmini uwezekano wa kumpandisha kwenye timu ya wakubwa endapo ataonyesha kiwango kikubwa.

Kinda huyo ni miongoni mwa wachezaji waliotoka Azam FC kwenda kufanya majaribio AIK, ikiwa ni matunda ya ushirikiano kati ya klabu hizo mbili unaolenga kubadilishana uzoefu na kukuza vipaji vya vijana.