Muhas, wadau wajadili  mtaala mpya wa usimamizi na ugavi bidhaa za afya

Morogoro. Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kimeanza kujadili, kuboresha na kuidhinisha mtaala mpya wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wa bidhaa za afya (HSCM).

Akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika mjini Morogoro, Mratibu wa Mradi wa Senselet Tanzania kutoka shule ya famasia Muhimbili, Profesa Eliangiringa Kaale amesema kikao kazi hicho kinawakutanisha wadau kutoka serikalini, taasisi za udhibiti, vyuo vikuu, washirika wa maendeleo, pamoja na sekta binafsi.

Amesema lengo ni kukubaliana kwa pamoja juu ya ujuzi, uwezo na mifumo inayohitajika kuimarisha usimamizi wa bidhaa za afya nchini Tanzania.

“Hili ni jukwaa la kimkakati la kitaifa, siyo mkutano wa kawaida wa kitaaluma na kwamba kabla ya kuandaa kwa mtaala huo, wadau likiwemo Shirika lisilokuwa na kiserikali la KUHNE Foundation lenye makao makuu nchini Ujerumani na ‘novo nordisk’ waliunga mkono,” amesema Profesa Kaale.

Amesema changamoto katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya husababisha kukosekana kwa dawa muhimu hospitalini, ucheleweshaji wa usambazaji wa vifaa tiba, upotevu wa rasilimali na matumizi yasiyo na tija hivyo mpango huo unalenga kutatua changamoto hizo kuanzia kwenye mzizi wake.

Aidha amesema kukamilika na kutumika kwa mtaala huo, kutajenga wataalamu mahiri watakaosimamia kwa ufanisi mnyororo mzima wa ugavi wa bidhaa za afya kuanzia upangaji, ununuzi, uhifadhi hadi usambazaji unaotumia takwimu na mifumo ya kisasa.

Profesa Kaale amesema mkutano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa afya nchini Tanzania, kwa kujenga wataalamu wabobezi wa usimamizi wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kupitia elimu, ushirikiano na mifumo madhubuti.

Awali akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Mfamasia Mkuu wa Serikali, Ofisa kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Ambwene Mwakalobo amesema kwa sasa nchi imepiga hatua katika eneo la usambazaji na ugavi wa bidhaa za afya.

Mwakalobo amesema hatua hiyo ya uboreshaji wa mtaala eneo la ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya utakaofundishwa Muhas, utawezesha kupatikana kwa wataalamu wabobezi kwenye mnyororo wa ugavi na usambazi wa bidhaa za afya.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wafamasia nchini, Fadhili Hezekiah amesema hali iliyopo kwa sasa kwenye mfumo mzima wa afya Tanzania inaridhisha, hivyo uboreshaji kwa mtaala huo eneo la ugavi na usambazi wa bidhaa za afya utafanya wataalamu wa afya kupata elelewa mpana wa ugavi na usambazaji.

“Zamani wataalamu wa famasia walikuwa wakifundishwa yale yanayohusu taaluma tu, hivyo kuwepo kwa mtaala huu kutasaidia kupatikana kwa dawa na vifaa tiba kwa wakati na utoshelezi na hivyo kuokoa fedha zinazotumika kununua bidhaa za afya ambazo hazihitajiki kwa sasa,” amesema Hezekiah.

Ameongeza, “Mtaala huu pia utasaidia wataalamu kujua mahitaji na matumizi ya dawa na hii itasaidia kupunguza changamoto ya kuharibika kwa dawa au vifaa tiba kukaa hadi kumalizika kwa muda wa matumizi.”

Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la KUHNE Foundation Tanzania la nchini Ujerumani, Dk Beatrice Millu amesema wameamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mtaala huo ili kuona jamii inapata huduma bora za afya.