KLABU ya Mbeya Kwanza imefikia makubaliano ya kumuajiri, Saad Kawemba ili awe Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) baada ya pande mbili kufikia uamuzi huo, ikiwa ni pendekezo la mmiliki wa kikosi hicho chenye makazi yake mjini Tabora, Yusuph Kitumbo.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Mbeya Kwanza, umeliambia Mwanaspoti, Kawemba amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ofa nzuri, licha ya hapo awali kutaka kurejea tena Mtibwa Sugar iliyopo Ligi Kuu Bara iliyoonyesha nia ya kumuhitaji ili akawe pia mtendaji mkuu.
Kawemba aliyewahi kufanya kazi ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar na Azam FC, kisha baadaye Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, ana uzoefu mkubwa, jambo lililomvutia pia Kitumbo kumchukua kutokana na mchango wake katika maeneo mbalimbali.
Mbeya Kwanza inayotumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kwa sasa katika mechi za nyumbani msimu huu za Championship, inapambana kurejea tena Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka daraja msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani na pointi zake 25.
Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza ya 15 na pointi 28, ingawa kwa msimu huu wa 2025-2026 ikishika nafasi ya tatu na pointi 40.