Serikali yataka matumizi ya mfumo wa anwani za makazi nchi nzima

Dar es Salaam. Serikali imezitaka taasisi zote za umma na binafsi kuanza kutumia mfumo wa kitaifa wa anwani za makazi, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha mwelekeo wa taifa kuelekea uchumi wa kidijitali.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angelah Kairuki, amebainisha hayo alipomwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi yaliyofanyika leo Jumapili, Februari 8, 2026, jijini Dar es Salaam.

Kairuki amesema Waziri Mkuu ameagiza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuweka taratibu madhubuti zitakazohakikisha utekelezaji bora wa mfumo huo katika sekta zote nchini.

Pia, ameziagiza mamlaka zote za serikali za mitaa kukusanya taarifa sahihi za makazi, ili kusaidia uundaji wa hifadhi data ya kuaminika ya anwani za makazi.

Kairuki amesema mfumo wa anwani za makazi hurahisisha utoaji wa huduma za umma na binafsi, na tayari umevutia mataifa mengine yanayotaka kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania.

Amesema mfumo huo, unaotekelezwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mujibu wa Sera ya Posta ya mwaka 2003, ni nyenzo muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma, biashara mtandaoni, usalama na ulinzi wa wananchi.

“Mfumo huu pia ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia, unaoungwa mkono na miundombinu ya uhakika ya usafiri na mifumo ya taarifa.

“Ufahamu wa mahali anapoishi kila mwananchi hurahisisha mipango, utoaji wa huduma na hatua za dharura,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdullah, amesema Serikali itaendelea kusimamia Mfuko wa Anwani za Makazi ili kuhakikisha uendelevu wa mfumo huo.

Amesema uwezo wa kutoa huduma bora unategemea mazingira wezeshi na mifumo imara ya utoaji wa huduma, akibainisha kuwa idadi ya anwani za makazi imeongezeka na kufikia milioni 12.9 kutoka milioni 12.8.

Amesema mfumo huo umeunganishwa na taasisi nyingine za Serikali, akibainisha mchango wake katika kuendeleza uchumi wa kidijitali.

“Tunakifanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumepima na kuchora ramani ya nchi nzima, na hivi karibuni tutazindua programu ya utalii itakayosaidia kukuza sekta hiyo,” amesema.

Amesema taasisi mbalimbali zimeanza kutumia taarifa za anwani za makazi, ikiwamo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Jeshi la Zimamoto.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anayeshughulikia Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, amesema sensa ya watu na makazi pamoja na sensa ya anwani imerahisisha utambuzi wa maeneo.

Amesema awali kulikuwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wananchi kutokana na uelewa mdogo, lakini hali ilibadilika baada ya kampeni za elimu kutolewa.