Vijana wa UVCCM Kinondoni watakiwa kujiendeleza kielimu

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe, Geofrey Timoth amewataka wajumbe wa Baraza la Kikanuni la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kujikita katika kujiendeleza kielimu na kuongeza ujuzi ili wawe tayari kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo.

“Ni muhimu vijana kuwekeza katika elimu na ujuzi, kwa sababu fursa nyingi zinapokuja zinahitaji mtu aliyekwisha jiandaa kitaaluma. Elimu ndiyo itakayowawezesha kushindana na kuchangamkia nafasi hizo,” amesema Timoth.

Timoth ametoa wito huo wakati akifunga Baraza la Kikanuni la UVCCM Wilaya ya Kinondoni lililofanyika jana, Februari 7, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Ameongeza kuwa dunia ya sasa inakwenda kwa kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, hali inayowalazimu vijana kuwa na maarifa ya kutosha ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameushukuru Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Kinondoni kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi cha kura za maoni na uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, uliokipatia CCM ushindi  katika Wilaya ya Kinondoni.

Pia aliupongeza uongozi wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni chini ya Mwenyekiti wake, Abdrahamani Abdallah Kassim, kwa kufanikisha upatikanaji wa madiwani saba vijana.

Timoth ameeleza kuwa yupo tayari kuendelea kushirikiana kwa karibu na vijana wa jumuiya hiyo katika kutatua changamoto zao, huku akisisitiza mshikamano na ushirikiano kama msingi wa maendeleo.

Vilevile, aliwahimiza vijana kuendelea kuyasema na kuyaunga mkono mafanikio na jitihada zinazotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa maslahi ya Taifa.