Haydom. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Regina Ndege amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wa nchi ili waongoze kwa busara, kumcha Mungu na kuwahudumia wananchi kwa haki na uadilifu.
Ndege ameueleza hayo leo Jumapili Februari 8, 2026 usharika wa Haydom Dayosisi ya Mbulu mkoani Manyara, alipokutana na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakiongozwa na Mkuu wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa.
Ndege amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na viongozi wa dini katika kuzidi kulijenga Taifa imara, lenye mshikamano, upendo na amani.
“Maendeleo, haki, amani na ustawi wa Taifa vinategemea kwa kiasi kikubwa mchango wa viongozi wa dini, kwa kuwa maombi yenu ni nguzo muhimu katika kudumisha mshikamano na utulivu wa nchi,” amesema Ndege.
Ameeleza kwamba Taifa la Tanzania, viongozi wake na wananchi kwa ujumla wanategemea maombi ya viongozi wa dini ili liendelee kumea, kustawi, kupiga hatua na kuwa na umoja zaidi.
“Ukiona Taifa limesimama, ujue viongozi wa dini wamesimama, maombi yenu yamekuwa msingi wa amani na umoja tulionao nchini,” amesema Ndege.
Hata hivyo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuthamini na kushirikiana na viongozi wa dini katika juhudi za kujenga Taifa lenye maadili, mshikamano na heshima kwa utu wa mwanadamu.
“Nawaomba wachungaji na maaskofu wa madhehebu mbalimbali kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wa nchi ili waongoze kwa busara, kumcha Mungu na kuwahudumia wananchi kwa haki na uadilifu,” amesema Ndege.
Dk Malasusa, amempongeza Ndege kwa kuonyesha uongozi unaojali masuala ya kiroho na mshikamano wa Kitaifa.
Amesisitiza kuwa kanisa hilo litaendelea kushirikiana na Serikali, katika kudumisha amani na kuimarisha maadili katika jamii.
Mmoja wa waumini wa KKKT usharika wa Haydom, Elizabeth Ombay amemshukuru Ndege kwa kujumuika nao katika kanisa hilo na kusali pamoja kwenye eneo hilo.