Bajaji, pikipiki zinazotumia umeme janga jipya la usalama Tanzania

Dar/Dodoma. Idadi kubwa ya bajaji na pikipiki zinazotumia umeme zinazofanya shughuli zake Dar es Salaam na Dodoma zinaendeshwa bila kusajiliwa, kuwa na bima, wala kubandikwa namba za usajili, licha ya matakwa ya kisheria, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Hali hiyo inawaweka wakazi wa miji hiyo katika hatari kubwa ya ajali na uhalifu unaozuilika, kwani wahalifu wanaweza kushiriki matukio ya kihalifu na kutokomea kwa urahisi.

Ripoti ya Takwimu za Matukio ya Uhalifu na Ajali za Barabarani ya 2025 inaonyesha kuwa kati ya Januari na Desemba 2024, Tanzania iliripoti ajali 1,735, zikiwa ni zaidi ya ajali 1,733 zilizoripotiwa mwaka 2023.

Ripoti hiyo, iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania, inaonyesha kuwa watu 1,715 walikufa huku 2,719 wakijeruhiwa katika matukio yaliyoorodheshwa 2024, ikilinganishwa na vifo 1,647 na majeruhi 2,716 mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya ajali za pikipiki 259 ziliripotiwa kitaifa kati ya Januari na Juni 2024, kutoka 216 kipindi kama hicho mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 19.9.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani viliongezeka kutoka 191 hadi 223, ongezeko la asilimia 16.7, huku Temeke, Kinondoni (zote ziko mkoani Dar es Salaam) na Mkoa wa Dodoma zikiongoza kwa idadi kubwa ya vifo hivyo.

Ripoti ya Africa E-Mobility 2025: Mwelekeo, Sera, na Uwekezaji katika Usafirishaji wa Vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme inaonyesha kuwa pikipiki na bajaji zimetawala soko la Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiongoza hasa kwa matumizi ya bajaji na pikipiki.

Ripoti hiyo inasema uingiaji wa pikipiki zinazotumia umeme (E2W) kwa matumizi ya kibiashara umechochewa na ongezeko la mahitaji, hali inayoiweka Afrika katika nafasi ya ukuaji wa usafirishaji unaoweza kupanuka katikati ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Licha ya dunia kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi, kuenea kwa haraka kwa usafirishaji kupitia vyombo vinavyotumia umeme kumesababisha bajaji na pikipiki kuongezeka barabarani katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma, hali inayohitaji kuchukuliwa utekelezaji wa haraka wa sheria.

Hii ni kinyume na Kifungu cha 57(b)(I–IV) cha Sheria ya Marekebisho ya Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Magari, Sura ya 124 ya mwaka 2023, ambacho kinatambua uwepo wa vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme ikiwa ni pamoja na pikipiki na bajaji katika mfumo wa kisheria wa Tanzania.

Pia, inakiuka Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, hasa Kanuni za Marekebisho ya Usajili wa Magari ya 2025, ambazo zilianzisha vifungu vidogo 1A(a)–(d).

Vifungu hivi vinaweka ada za leseni za magari zinazotozwa wakati wa utoaji wa cheti cha usajili kwa vyombo vinavyotumia umeme.

Ada hizo zimegawanywa katika makundi matatu: EVs za Nguvu Ndogo (chini ya 50kWh), EVs za Nguvu ya Kati (50.1–100kWh) na EVs za Nguvu Kubwa (100.1–200kWh).

Kanuni hizo, zilizotangazwa rasmi tarehe 26 Juni 2025 na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, zinaweka ada za usajili za Sh50,000, Sh200,000 na Sh250,000 kwa madaraja ya 1, 2 na 3 mtawalia, huku Sh300,000 zikihusika kwa EVs za utendaji wa juu.

Kifungu kidogo cha 1B kinaeleza kuwa ada ya leseni ya pikipiki, iwe ya umeme au ya kawaida, ni Sh30,000, wakati ile ya bajaji inayobeba mizigo au abiria ni Sh50,000.

Hata hivyo, Kifungu cha 13(1) na (2) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, kinakataza matumizi ya gari au trela yoyote kwenye barabara za Tanzania pasipo kusajiliwa.

Kifungu cha 13(2) kinasema kwamba mmiliki au dereva yeyote anayeendesha gari lisilosajiliwa anafanya kosa hivyo kustahili faini isiyozidi Sh50,000, kifungo cha hadi miaka mitano, au vyote viwili, na chombo chake kinaweza kutaifishwa na Serikali.

Hali ya sasa pia inakiuka Mpango Mkakati wa Taifa wa Usalama Barabarani wa 2024/25-206/27 na ahadi ya Tanzania katika Muongo wa Dunia wa Hatua za Usalama Barabarani 2021–2030.

Pia, Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) umelenga kupunguza vifo na majeruhi wanaotokana na ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo 2030.

Matokeo ya utafiti wa Mwananchi yanaonyesha kuwa Dar es Salaam, kitovu cha biashara, na Dodoma, mji mkuu wa kiutawala, imeendelea kukabiliwa na changamoto kubwa.

Miji hiyo imekumbwa na ongezeko la vyombo hivyo visivyosajiliwa hali inayochangia kuongezeka kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama kutokana na ajali za barabarani, kuwezekano wa kuongezeka kwa matukio ya uhalifu, na upotevu wa mapato kutokana na faini na adhabu zisizokusanywa.

Katika utafiti wake wa Oktoba hadi Desemba 2025 katika maeneo ya Kariakoo, Kimara, Tabata, Kitumbini jijini Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya mkoani Dodoma, Mwananchi limebaini uwepo wa bajaji na pikipiki nyingi zinazotumia nishati ya umeme zinazofanya shughuli zake bila kusajiliwa.

Baadhi zinatumika kwa usafirishaji wa jumla, huku zikiendeshwa na kupita barabara zenye msongamano na mitaa ya majiji hayo bila kikwazo wala kuhojiwa kuhusu kukosekana kwa namba za usajili.

Katika mahojiano na waendeshaji, walisema hawajawahi kusimamishwa na polisi au vyombo vya usalama na kuombwa nyaraka za usajili.

Wengine walisema hawajui kama usajili wa vyombo hivyo ni jambo la lazima, huku wengine wakidai wauzaji waliwaeleza kuwa vyombo hivyo “viko kama baiskeli” hivyo havifungwi na sharti la usajili wala kuwepo kwa nyaraka.

Wengi walikiri kuwa kwa kuwa hawajawahi kuhojiwa na mamlaka kuhusu usajili, hawakuona sababu ya kusajili vyombo hivyo vinavyotumia umeme.