MKUU wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuweka jitihada za kununua mbwa wapya wa kisasa na wenye uwezo ili kuboresha muonekano wa mbwa wa Polisi mwenye umbo lenye kumdhoofisha mhalifu.
IGP Wambura, ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wakuu wa Kikosi cha Mbwa na farasi wa Mikoa na Wataalam Waongoza Mbwa na Farasi kikao kilichofanyika jijini Dar es salaam Februari 9,2026 huku akiweka msisitizo kwenye eneo la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwatumia Wanyama kazi katika kudhibiti uhalifu kwenye maeneo yao.
Akizungumza na Watendaji hao IGP Wambura, amebainisha kuwa, Kikosi hicho kina umuhimu mkubwa kiusalama kwa kuwa Doria za mipakani na maeneo mengine muhimu hulazimika kutumia mbwa na farasi kwani ni rahisi kupenya kwenye maeneo ambayo gari haliwezi kupita kwa urahisi.
Amesema, Jeshi la Polisi lina Mbwa na Farasi wanaofanya kazi katika bandari, viwanja vya ndege na mipakani kwa lengo la kuzuia biashara za magendo na usafirishaji haramu wa silaha pamoja na dawa za kulevya, hivyo amewataka kuendelea kuweka nguvu ya kutosha kuhakikisha kuwa, muda wote mipaka yetu inakuwa salama kwa kushirikiana na askari kutoka vikosi vingine ili kudhibiti uhalifu.
Aidha, IGP Wambura, ametoa wito kwa Watendaji wa Kikosi hicho hususani tunapojiandaa na mashindano ya AFCON 2027 ambapo Tanzania ni mojawapo ya nchi Mwenyeji wa Mashindano hayo, kuhakikisha wanakuwa na mbwa na farasi bora wenye mafunzo ya viwango vya kimataifa ili waweze kutoa huduma bora isiyokuwa na mashaka na ambayo itasaidia kuiletea sifa nchi yetu.
Nae Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Awadhi Juma Haji, amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuboresha kikosi cha Mbwa na Farasi na kuhakikisha kikosi kinatekeleza majukumu yake ipasavyo ya kukabiliana na matukio mbalimbali ya kihalifu ikiwemo udhibiti wa dawa za kulevya, silaha haramu pamoja na bidhaa nyingine za magendo.
Kamishna Awadhi amesema kikosi hicho kimeweza kushiriki kwenye operesheni za matukio mbalimbali ikiwemo mikutano ya kitaifa na kimataifa ili kuimarisha amani na utulivu wa kutosha na kudhibiti viashiria vyovyote vya kihalifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Mbwa na Farasi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Namsemba Mwakatobe, amesema kikao kazi hiki kitawezesha kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo wa kiutendaji hivyo washiriki wa kikao kazi hicho wataenda kuleta mabadiliko ya kiutendaji kwenye maeneo yao kwa kuhakikisha wanadhibiti uhalifu.




