Dar es Salaam. Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo inatarajiwa kuendelea kuunguruma, ambapo upande wa mashtaka utajibu hoja za kisheria za pingamizi la Lissu kuhusiana na uhalali wa mashahidi fiche wa Jamhuri.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea leo Jumatatu, Februari 9, 2026 kwa siku 20 mfululizo za kazi, mpaka Machi 6, 2026.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mara ya mwisho kesi hiyo iliahirishwa Novemba 12, 2025 baada ya kumalizika kwa kikao (session) cha usikilizwaji wa kesi hiyo kilichoanza Septemba 8, 2025, ambapo mashahidi watatu wa Jamhuri, wote wakiwa ni maofisa wa Polisi, walitoa ushahidi wao.
Siku hiyo, upande wa mashtaka ulimleta shahidi wake wa nne, ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri katika kesi hiyo.
Mashahidi hao fiche ni raia wa kawaida (wasio askari), ambao Mahakama Kuu iliamuru wapewe ulinzi, kufuatia maombi ya Jamhuri kwa madai kuwa wamekuwa wakitishiwa usalama wao.
Mahakama hiyo, katika uamuzi huo uliotolewa na Jaji Hussein Mtembwa Agosti 4, 2025, ilielekeza mashahidi hao majina yao yasitajwe, wala anuani za makazi yao au taarifa zitakazofanya watambulike wao, familia zao au watu wao wa karibu.
Pia ilizuia kusambazwa kwa maelezo yao au nyaraka zozote zinazowahusu zinazoweza kusababisha wakatambulika bila idhini ya mahakama, huku pia ikielekeza kutumia majina bandia wakati wote wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Jamhuri ilipeleka mahakamani hapo maombi ya ulinzi wa mashahidi hao chini ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za Mwaka 2025, zilizotungwa na Jaji Mkuu kwa mujibu wa kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, siku hiyo, wakati shahidi huyo wa nne wa upande wa mashtaka aliyetambulishwa kwa jina la P11 akiwa tayari katika kizimba maalumu kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake, Lissu aliibua pingamizi la awali la hoja za kisheria.
Katika pingamizi hilo, Lissu alitoa hoja sita kupinga shahidi huyo na wengine wa aina hiyo kutoa ushahidi wakiwa kifichoni.
Baada ya Lissu kumaliza hoja zake, Jamhuri iliomba muda wa kuandaa majibu ya hoja za Lissu. Hata hivyo, kwa kuwa siku hiyo ilikuwa mwisho wa kikao cha usikilizwaji wa kesi hiyo, iliahirishwa kusubiri kupangiwa tarehe nyingine katika kikao kingine.
Hoja za pingamizi la Lissu
Mosi, Lissu alidai katika kizimba cha ushahidi alikokuwa shahidi huyo, mahakama ilikuwa haiwezi kumuona, kinyume na kanuni ya 3 ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni hiyo, kizimba ni sehemu ya shahidi kusimama au kukaa wakati wa kutoa ushahidi bila kuonekana isipokuwa kwa jaji au hakimu, lakini alidai kuwa mahali alikokuwa shahidi huyo hata mahakama (majaji) walikuwa hawamuoni.
Mbili, Lissu alidai shahidi huyo hajabainishwa katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani.
Alifafanua kwamba kwa mujibu wa kanuni ya 5(1) ya kanuni hizo, Mahakama inaweza kutoa amri ya ulinzi iwapo itaridhika kuwa mtu aliyebainishwa katika maombi ni shahidi katika shauri husika na maisha yake au usalama wake uko hatarini.
Alidai kuwa mtu aliyebainishwa ni yule aliyetajwa, lakini akadai kuwa katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani, katika viapo vyote viwili vilivyounga mkono maombi hayo, hakuna hata kimoja kilichotaja jina la shahidi hata mmoja, wala waliokuwa wanawatishia, wala hata aina ya vitisho.
Tatu, Lissu alidai hakuna mahali ambako mahakama ilitoa amri ya matumizi ya kizimba maalumu, na kwamba hata upande wa mashtaka hawakuwa wameliomba hilo, hivyo hawawezi kupata kile ambacho hawakukiomba.
Nne, alidai matumizi ya kizimba maalumu yanaathiri haki ya kusikilizwa kwa usawa kinyume na kanuni ya 6(2) na 5(f) za kanuni hizo.
Alihoji shahidi akitoa ushahidi kwenye kesi kubwa kama hiyo bila mahakama kumfahamu wala washtakiwa isipokuwa waendesha mashtaka, hiyo inawezaje kuwa usikilizwaji wa haki, na mahakama itatoaje uamuzi wa haki?
Tano, Lissu alidai kuwa sheria inayotoa ulinzi wa mashahidi ambayo kwayo kanuni za ulinzi wa mashahidi zimetengenezwa ni batili kwa kuwa haijawahi kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 7 ya Mwaka 2018, iliyoanzisha kifungu cha 194 cha Sheria ya CPA kinachozungumzia ulinzi wa mashahidi, haijawahi kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Kifungu cha 14 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria kinasema ili sheria ianze kutumika lazima iwe imechapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Alidai ikitangazwa itaonekana katika tovuti na maktaba za Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais – Utumishi, Mahakama na Bunge, Duka la Vitabu vya Serikali, Maktaba na Hansard za Bunge, lakini huko kote haipo.
Katika hoja ya sita, alidai kuwa kanuni hizo haziwezi kutumika katika kesi yake, kwani zilitungwa wakati tayari kesi hiyo ikiwa imeshaanza.
Alibainisha kuwa kanuni hizo zilichapishwa Julai 11, 2025 wakati kesi hiyo ilianza Aprili, miezi mitatu kabla, na kwamba sheria inaanza kutumika siku inapochapishwa au tarehe nyingine yoyote, na kwamba haiwezi kuanza kutumika kwa kurudi nyuma.
Hivyo alidai kuwa mahakama ikiruhusu utaratibu huo, hawawezi kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za mahakama, kwani haijulikani kama shahidi huyo ni huyo huyo, hawajui kama anasoma ushahidi wala kama anatumiwa meseji.