Kesi ya uporaji mamilioni NMB Temeke, Polisi kuuawa kusikilizwa upya

Dar es Salaam. Unalikumbuka tukio la wizi wa kutumia silaha katika Benki ya NMB Temeke, jijini Dar es Salaam la mwaka 2009 lililoambatana na mauaji ya askari Polisi na mlinzi wa kampuni binafsi? Sasa shauri hilo la mauaji litasikilizwa upya.

Hii ni baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoketi jijini Dar es Salaam kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya, ikiwa imeshachukua miaka 17 tangu tukio la mauaji, na usikilizwaji huo upya ni wa pili kuamriwa na mahakama.

Hii ni baada ya jopo hilo, lililoundwa na majaji Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Dk Deo Nangela, kubaini dosari za kisheria kwamba taarifa aliyosomewa mshtakiwa wakati kesi iliposikilizwa upya zilikuwa ni tofauti na zile za awali.

Katika hukumu yao waliyoitoa Februari 6, 2026, majaji hao walisema taarifa ya kosa hilo iliyowasilishwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa, aliyesikiliza upya shauri hilo, ilikuwa ni tofauti na iliyokuwa imewasilishwa mbele ya Jaji Salvatory Bongole.

Walitoa hukumu hiyo katika rufaa iliyokatwa na mrufani Richard Muhanza, aliyehukumiwa adhabu ya kifo Novemba 21, 2018 kwa kosa la kumuua Koplo Joseph Milambo mwenye namba E.329 na mlinzi wa kampuni binafsi, Seif Mkwike.

Tukio hilo lilitokea Julai 31, 2009 asubuhi, ambapo kundi la majambazi wenye silaha za moto walivamia Benki ya NMB tawi la Temeke kwa lengo la kupora fedha. Walipofika tu, walianza kuwamiminia risasi polisi waliokuwa zamu.

Hii ilisababisha majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi hao, na ni katika majibizano hayo, Koplo Milambo aliuawa pamoja na Mkwike. Katika purukushani hizo, majambazi hao walirusha bomu la kutupwa kwa mkono kuelekea kwa polisi.

Baadaye majambazi hao walifanikiwa kuingia ndani ya benki na kupora kiasi cha fedha ambacho hakikuwekwa wazi, ambapo katika uchunguzi wa tukio hilo, polisi walimkamata Muhanza na watu wengine wanane wakashtakiwa kwa mauaji.

Walifikishwa mahakamani katika kesi ya mauaji namba 22 ya mwaka 2011, ambayo ilisikilizwa na Jaji Bongole, na Julai 28, 2016 alitoa hukumu iliyowatia hatiani washtakiwa wanne, akiwamo Muhanza, na kuwahukumu adhabu ya kifo.

Rufani ilivyowatema watatu

Hawakuridhika na hukumu hiyo na walikata rufaa Mahakama ya Rufani kupitia rufaa namba 504 ya mwaka 2016. Oktoba 12, 2017, jopo la majaji waliosikiliza rufaa hiyo wakaamuru shauri hilo lisikilizwe upya.

Hii ni baada ya kubaini kuwa shauri hilo lilisikilizwa bila uwepo wa wazee washauri wa mahakama (assessors), ambalo lilikuwa ni takwa la lazima la sheria, hivyo wakabatilisha hukumu na wakaagiza lisikilizwe mbele ya jaji mwingine.

Katika kutekeleza amri hiyo ya mahakama, kesi hiyo ikapelekwa kwa Jaji Matupa, lakini hati ya mashtaka na taarifa za kosa alizosomewa mshtakiwa zilikuwa na washtakiwa wanne badala ya washtakiwa wale tisa katika kesi ya mwanzo.

Katika hukumu yake, Jaji Matupa aliwaachia washtakiwa watatu na kumtia hatiani mrufani na kumhukumu adhabu ya kifom, lakini hakuridhishwa na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa akiegemea sababu 11, akitaka aachiliwe huru na mahakama.

Dosari ya kisheria inabainika

Katika usikilizwaji, mrufani aliwakilishwa na wakili Mluge Fabian, wakati upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Deborah Mushi.

Katika usikilizwaji huo, mahakama ikawataka mawakili hao kufanya mawasilisho ya iwapo amri ile ya Mahakama ya Rufani iliyotolewa Oktoba 12, 2017 ya kesi hiyo kusikilizwa upya ilitekelezwa na mahakama.

Katika kujibu hoja hiyo, wakili Mluge alisema kesi ya marudio ilikuwa na dosari, kwani ilisikilizwa kwa taarifa zisizo sahihi na kufafanua kuwa taarifa zilizokuwa mbele ya Jaji Matupa, aliyesikiliza upya shauri hilo, zilikuwa ni tofauti na za Jaji Bongole.

Alijenga hoja kuwa kisheria, usikilizwaji upya wa shauri unataka urudiwe katika hati ile ile ya mashtaka au taarifa ya shauri lililoamriwa lisikilizwe upya, lakini katika shauri hilo, usikilizwaji upya uliegemea katika taarifa tofauti na za awali.

Wakili huyo akasema kwa kuwa kuna baadhi ya nyaraka zinakosekana kwenye jalada, basi mahakama inachoweza kufanya ni kubatilisha mwenendo, hukumu na adhabu aliyopewa mrufani na kuachiliwa huru, na siyo kesi kusikilizwa upya.

Kwa upande wake, wakili Mushi alikuwa na maoni yanayofanana na ya wakili Mluge kuwa amri ya mahakama ya shauri hilo kusikilizwa upya haikutekelezwa, kwani lilisikilizwa upya lakini kwa kuegemea taarifa tofauti na za awali.

Hata hivyo, alisema si sawa kuulaumu upande wa Jamhuri pekee kwa makosa hayo na kusema ingawa taarifa za kosa zilizowasilishwa mahakamani zilikuwa si sahihi, kosa lisiwe kwa hasara ya watu waliokufa katika mauaji hayo.

Alisema kwa kusawazisha mizani na kuzingatia mambo hayo yote, amri ya kurudiwa kwa shauri (retrial) ingetimiza matakwa ya haki katika mazingira hayo, kwani kufanya hivyo kutaonekana kama haki imetendeka kwa pande zote mbili.

Katika hukumu yao, majaji hao walisema ni jambo lililo wazi kuwa maelezo waliyosomewa washtakiwa wakati kesi iliposikilizwa upya yalikuwa ni tofauti na yale ambayo yalisomwa wakati kesi hiyo iliposikilizwa mara ya kwanza.

“Hii ni kwa sababu maelezo ya awali yaliyokuwa mbele ya Jaji Bongole yalikuwa na washtakiwa tisa, lakini yaliyosomwa mbele ya Jaji Matupa, ambayo ndiyo msingi wa rufaa hii, yalikuwa na washtakiwa wanne,” wanasema majaji hao katika hukumu yao.

“Katika mazingira hayo, tunakubaliana na hoja za mawakili wa pande zote mbili katika shauri hili kwamba maelezo ya kosa yaliyotolewa wakati kesi iliporudiwa kusikilizwa yalikuwa na dosari, hivyo amri ya mahakama haikutekelezwa.”

Majaji hao walisema neno ‘retrial’ (kusikilizwa upya kwa kesi) linamaanisha shauri hilo lisikilizwe upya kama vile halijawahi kusikilizwa, na wakatoa mifano ya hukumu za kesi mbalimbali zilizolitafsiri neno hilo kwa maana hiyo waliyoitafsiri.

“Kwa kuegemea uamuzi wa mashauri tuliyoyanukuu, tuna msimamo thabiti kwamba kuingiza taarifa au ushahidi mpya wakati wa kurudia kusikiliza shauri (retrial) haikuwa sahihi kisheria,” walisisitiza majaji hao katika hukumu yao hiyo.

“Inasisitizwa, mahakama iliyosikiliza kesi upya ilitakiwa kuanza mwenendo wa shauri kwa kusababisha maelezo ya awali yasomwe kwa washtakiwa tisa waliopita. Tofauti na hivyo, amri ya mahakama haikutekelezwa.”

Majaji hao walisema maelezo au taarifa hizo zilizosomwa wakati wa usikilizaji upya wa shauri zingekuwa halali tu kama kungefanyika marekebisho kwanza (amendment) chini ya kifungu cha 276(2), ambacho sasa ni 294 cha CPA.

“Bahati mbaya hili halikufanywa na mahakama wala upande wa Jamhuri. Kwa dosari hizo, hatuwezi kusema kwamba mrufani alishtakiwa kihalali na kutiwa hatiani, kwa sababu yote yaliyotokea mbele ya mahakama yalikuwa batili.”

Majaji hao walisema wamezingatia mawasilisho ya mawakili wa pande zote juu ya nini kifanyike, ama kesi isikilizwe upya au mshtakiwa aachiwe huru, na kwamba wanatambua kesi hiyo ni ya muda mrefu na mrufani yuko gerezani miaka 17.

“Tunaelewa pia kama tutaamuru kesi isikilizwe upya itakuwa ni mara ya pili, lakini ni msimamo wa sheria kuwa kesi inaweza kuamriwa kusikilizwa zaidi ya mara moja pale ambapo mazingira ya kufanya hivyo yanataka iwe hivyo,” walisema.

“Pamoja na kwamba tunaweza kusikitikia hali ya mrufani (kukaa muda mrefu gerezani), bado tuna msimamo thabiti kwamba, kwa mazingira ya kesi hii, itakuwa ni kwa manufaa ya haki kuamuru isikilizwe tena upya,” walisisitiza majaji hao.

Majaji hao walisema wanaamuru hivyo ili kutii amri ya mahakama iliyotolewa Oktoba 12, 2017 katika shauri la rufaa namba 504 la 2016, na wakaagiza kesi hiyo irudiwe kusikilizwa kwa haraka, na mrufani ataendelea kusalia mahabusu.