Madereva wataka Polisi iweke wazi kituo anachoshikiliwa kiongozi wao

Dar es Salaam. Uongozi wa Umoja wa Madereva wa Malori, Mabasi na IT–Tanzania (Tatamata) umelitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kuweka wazi kituo anachoshikiliwa mwenyekiti wao, Godlove Materu, ili familia, viongozi wa chama na mwanasheria wake wapate fursa ya kumuona na kufuatilia haki zake za kisheria.

Hatua hiyo imekuja baada ya jana Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kukiri kumshikilia Materu kwa tuhuma za makosa ya jinai ya kudaiwa kupanga matukio ya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe, kinyume na madai ya awali yaliyodai kwamba kiongozi huyo alitekwa na watu wasiojulikana.

Materu aliripotiwa kutekwa Februari 5, 2026, katika eneo la Chapwa, Tunduma mkoani Songwe, ambako alidaiwa kuchukuliwa na watu watatu waliovaa kiraia waliotumia gari aina ya Land Cruiser jeupe, baada ya kujifanya wateja katika kibanda chake cha biashara ya vinywaji.

Baada ya viongozi wa Tatamata kutoa siku mbili kwa Serikali, wakitishia kusitisha shughuli za usafirishaji iwapo kiongozi wao hatapatikana, Jeshi la Polisi lilizungumza na Mwananchi na kuthibitisha kuwa linamshikilia Materu kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, alisema Materu anashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo.

“Tunamshikilia kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo. Si muda mrefu tutatoa taarifa rasmi kwa umma, hasa kutokana na uvumi unaoenea mitandaoni,” alisema Kamanda Senga.

Hata hivyo, baada ya taarifa ya Jeshi la Polisi, leo Februari 9, 2026, Wakili wa Materu, Aloyce Komba, amesema taarifa za Polisi hazijajibu maswali ya msingi yanayohusu haki na usalama wa mteja wake.

“Taarifa ya Polisi haijaeleza ni lini mteja wetu alikamatwa, anashikiliwa kwa kosa gani wala yupo kituo gani. Familia, viongozi na mwanasheria wake hawajapewa taarifa rasmi,” amesema Komba.

Amesema Materu ameshikiliwa kwa takribani siku tano bila kufikishwa mahakamani, ni kinyume na matakwa ya sheria, huku wakishindwa kumuona licha ya kuzunguka vituo mbalimbali vya polisi mkoani Songwe.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Tatamata, Yohana Mwanyaga, amesema juhudi za kumtafuta Materu katika vituo vya polisi bado hazijafanikiwa, pamoja na kwamba polisi wamekiri kumshikilia.

“Kama ana tuhuma zozote, basi afikishwe mahakamani badala ya kushikiliwa bila taarifa huku familia yake ikihangaika,” amesema Mwanyaga.

Naye mke wa Materu, Martha Mushi, amesema baada ya kupata taarifa ya Polisi kumshikilia mumewe, wamezunguka vituo vyote bila mafanikio.

Katika maelezo yake jana kwa Mwananchi, Kamanda Senga aliwatoa wasiwasi ndugu na viongozi wa chama hicho, akisema wawe na amani kwani Materu yuko mikono salama, wakikamilisha shughuli za upelelezi.