Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda ameweka wazi kuwa Serikali imempitisha Kocha Miguel Gamondi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, kutokana na uwezo wake aliouonyesha kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 iliyofanyika Morocco.
Makonda ameyasema hayo leo Februari 9, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari alipofanya ukaguzi wa maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Kilichobaki kwa sasa ni kusubiri maamuzi ya Gamondi mwenyewe kuweka saini kuthibitisha kuwa yupo tayari kuitumikia Stars kuelekea AFCON 2027 kwani Serikali ina imani naye.
“Kuhusu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, kazi imebaki upande wa Miguel, Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tumeamua kubaki naye na malipo yake yote yatasimamiwa na Serikali.
Gamondi alikabidhiwa Stars kukaimu nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ na alifanikiwa kuandika historia ya kuifikisha timu hiyo hatua ya 16 bora kwenye michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika nchini Morocco huku Senegal ikifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco kwenye mchezo wa fainali.