KIKOSI cha Ruangwa Queens kimewapa mapumziko ya wiki mbili wachezaji pamoja na benchi la ufundi kabla ya kurejea kambini Februari 25, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujiimarisha zaidi kuelekea mechi zijayo za Ligi Kuu ya Wanawake.
Mapumziko hayo yamekuja wakati Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa imesimama kupisha kalenda ya FIFA, ambapo timu za Taifa zinashiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Katika kipindi hiki, timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania inaendelea na maandalizi ya kuwania fainali za Mataifa ya Afrika (WAFCON), ambako imepangwa kundi B, pia timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens ipo kwenye harakati za kuwania nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia.
Akizungumzia hilo, Nahodha wa Ruangwa Queens, Mwanahamisi Jaffar amesema kurejea kambini Februari 25 kutakuwa mwanzo mpya kwa kikosi hicho kufanya tathmini ya kina ya mwenendo wao kwenye mechi zilizopita.
Aliongeza, kipindi hicho kitaipa timu nafasi ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza, pamoja na kuweka sawa maeneo yote yaliyokuwa na changamoto na kurudi wakiwa imara.
“Kikosi kitarejea kambini terehe 25/02 hii itakuwa nafasi nyingine kwetu kurekebisha na kuweka sawa yale yote yaliyokuwa changamoto kwenye mechi zilizopita,” amesema nahodha huyo na kuongeza;
“Kama wachezaji tunatumia mapumziko haya ya wiki mbili kuweka akili na miili sawa tayari kwa mazoezi na mbinu mpya kutoka benchi la ufundi tunajua hatukuanza vizuri ligi kutokana na ugeni wetu.”