Samatta, Msuva mambo magumu | Mwanaspoti

LICHA ya nyota wawili Mbwana Samatta na Simon Msuva kuwa na umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars takwimu zinaonyesha msimu huu bado hawajaonyesha viwango vikubwa wakiwa kwenye klabu wanazozitumikia.

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta anayecheza katika Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1, akiwa na kikosi cha Le Havre safari yake imekuwa na changamoto kubwa.

Katika mechi 13 alizocheza msimu huu wa Ligi Kuu Ufaransa, mshambuliaji huyo bado hajafunga bao wala kutoa asisti tofauti na msimu uliopita alipokuwa PAOK ya Ugiriki.

Akiwa PAOK, Samatta alifunga mabao manne na kutoa asisti moja katika mechi 12, takwimu zilizothibitisha bado ana uwezo wa kumalizia nafasi.

Hata hivyo, ni kama uhamisho wake wa kwenda Le Havre umeambatana na ugumu wa ligi, kasi ya mechi na majukumu ya kucheza nafasi tofauti za ushambuliaji.

Samatta hatumiki kama mshambuliaji wa mwisho pekee mara nyingi hushuka chini kusaidia ujenzi wa mashambulizi, kufungua nafasi kwa wachezaji wa pembeni na kupambana na mabeki wenye nguvu.

Hilo limeathiri idadi ya nafasi anazopata za kufunga, lakini halijafuta mchango wake kiufundi ndani ya timu.

Ndiyo maana licha ya kutofunga mabao, benchi la ufundi la Le Havre limeendelea kumuamini, ishara kwamba nyota huyo anatoa zaidi ya kufunga.

Kwa Simon Msuva naye hali si shwari kwani msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa asisti nne katika mechi 12, tofauti na msimu uliopita alipofunga mabao 12 katika mechi 11.

Takwimu zinaonyesha msimu huu ameshuka hasa katika kufumania nyavu za wapinzani tofauti na msimu uliopita ambao alikuwa na wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi.

Hata hivyo, kubadilishiwa majukumu kwenye kikosi hicho imekuwa moja ya sababu ya nyota huyo kutoanza na makali akitumika zaidi kama mchezeshaji wa pembeni kuliko mshambuliaji.