Samia ataja sababu kuwaondoa wasaidizi wake Ikulu, mkeka wa Ma DC…

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema uamuzi wake wa kuwaondoa baadhi ya wasaidizi wake Ikulu na kuwapa nafasi nyingine serikalini, unalenga kuwakuza kwa kuwa ameshawalea na wanatosha kutumika kwa kazi nyingine.

Ufafanuzi wa mkuu huyo wa nchi, unakuja baada ya Februari 6, 2026 kumteua aliyekuwa Katibu wake binafsi, Balozi Waziri Salum, kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara.

Hata hivyo, Balozi Waziri si wa kwanza kuondolewa Ikulu kupelekwa wizarani. Wapo waliotangulia akiwemo Petro Magoti aliyekua Msaidizi wa Rais Siasa, akateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Mwingine ni Dk Blandina Kilama aliyekuwa Msaidizi wa Rais Uchumi, aliyeondolewa Ikulu na kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, huku Juma Mkomi aliyekuwa Katibu wake, alimpeleka serikalini na sasa ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Februari 9, 2026 alipozungumza katika hafla ya kuwaapisha wateule wake, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake hiyo, ameeleza amekaa na Balozi Waziri kwa muda mrefu na amefanya kazi nzuri, akisisitiza amemlea na kumkuza vya kutosha na sasa anampa nafasi nyingine akasukume kazi.

“Hiyo ndio kazi yangu kulea na kutoa na nimetoa wengi. Kuna kina Juma Nkomi saa hizi ni makatibu wakuu utumishi, nimetoa kina Magoti, mnakisikia huko kinanguruma.

“Kwa hiyo baba yangu (Balozi Waziri) nimekupeleka ukakue, lakini jingine unajua ninachokitaka, umekua na mimi kwa muda mrefu, kashirikiane na waziri wako nataka viwanda,” amesema.

Amemtaka akaanzie alipoishia Selemani Jafo, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, akisema atampima kwa idadi ya viwanda vitakavyoongezeka na kupanuka kwa biashara.

“Kama hamjafahamu Waziri unajua namna ya kunifikia mchukue mwenzio njooni tukae tueleweshane,” amesema.

Amesema ameona mambo mengi baada ya kumteua Balozi Waziri, lakini sababu ya uamuzi huo ni kumpeleka kwenye sekta akakue baada ya kumlea.

“Vinginevyo ningeacha adumae na mimi keshokutwa natoka future yake iko wapi, nimuache adumae na mimi hapa, anayekuja atakuja na wa kwake, kwa hiyo acheni midomo ya uongo,” amesema.

Kwa upande wa watendaji wengine waliokuwa Ikulu aliowateua, amesema wanajua yaliyoko ndani kwa kuwa amekuwa nao katika vikao vya baraza la mawaziri hivyo wakatekeleze yale waliyokua wakipendekeza.

Katika hotuba yake hiyo, alitoa maelekezo kwa Dk Toba Nguvila aliyemteua kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha (RAS), akisema alimwona alipoomba kwenda kugombea ubunge na alijua kuwa asingefanikiwa. Awali, alikuwa RAS wa Dar es Salaam.

“Nilijua hakika utakwenda kupigwa hurudi, lakini mtoto akililia wembe mpe ukishamchinja atajua. Kwa hiyo wembe umekuchinja mwanangu, nikasema ngoja upumzike kidogo, lakini utendaji wako naujua vizuri.

“Nakurudisha nakupeleka Arusha unaijua, imechangamka ina mambo mengi, Arusha ni taswira ya nchi yetu, tunahudumia taasisi za kikanda za kimataifa, nataka ukafanye kazi, nakuamini na najua unaweza, kanifanyie kazi Arusha,” amesema.

Kwa upande wa Dk Stephen Nindi, aliyemteua kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, amesema mkoa huo unategemewa kwa kilimo kwani unalisha Tanzania na unalima mazao ya biashara, akimtaka akamsaidie.

Ametaka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ihakikishe biashara ya Carbon Credit inainufaisha nchi.

“Carbon Credit fedha nyingi tunanyang’anywa watu wetu wanapata, ukiangalia Tanganyika wanapata wanajisifu tunapata mpaka Sh9 bilioni kwa Carbon Credit,” amesema.

Amesema wanaofaidika zaidi ni watu wa kati kwa kuwa wanachukua fedha nyingi, akiwataka wateule wake wakashirikiane kusimamia kituo cha Carbon Credit ili Tanzania ipate haki zake.

Kuhusu mifugo na uvuvi, amesema ni sekta muhimu kwa vijana na hivi karibuni alikaa na mawaziri na baadhi ya watu wanaotaka wawasaidie.

Amesema mifugo, uvuvi na kilimo ndizo sekta ambazo zikisimamiwa vema zitazalisha ajira kwa vijana wengi na kuleta mapato lukuki kwa Serikali.

Kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara, amesema kipimo cha watendaji wake ni kuifanya Tanzania ijitegemee si chini ya asilimia 70 kwa uzalishaji wa dawa.

“Najua kuna kazi imeanza kufanyika ya viwanda nenda kaisimamie, lakini muelewe wanaowekeza kina nani. Kuna wengi wanaotaka kuja Tanzania lakini wanakwamishwa na ardhi na ukiritimba wetu nataka ukasimame kufikia 2030 tujitegemee kwa asilimia si chini ya 80.

“Utasemwa mengi sijui wa Crown Radio, sijui nini sicho nilichokupelekea, najua unaweza, unaweza kusimamia viwanda vya dawa wawekezaji, nenda kasimamie,” amesema.

Rais Samia alianza kwa kuwazungumzia wakuu wa mikoa wapya aliowapisha ambao ni Kanali Yahya Kido wa Kagera na Kanali Donald Msengi wa Mtwara akisema ni mikoa ya kimkakati kwa ulinzi wa nchi na ndiyo maana amewatoa jeshini kutokana na umuhimu wake.

Amesema wakuu wa wilaya atakaowateua katika mikoa ya Kagera na Mtwara kuwa ni wale watakaoendana na wakuu wa mikoa aliowaapisha, kwani  ni mikoa muhimu na ya kimkakati lakini pia ulinzi na usalama wa nchi.

“Nitakupangieni ma-DC ambao mnaweza kwenda nao na lugha moja ili kwenda kuimarisha ulinzi katika mikoa ile, ni mikoa ya kimkakati kwetu…narudia ile miwili ni mikoa muhimu kwetu ndiyo maana nimetoa makanali jeshini nimewaleta huku,” amesema Samia.

Kwa upande wa Balozi Marko Gaguti aliyemteua kuwa balozi, amesema anakusudia kumpa mamlaka ya kuiwakilisha Tanzania katika Taifa lingine na atapelekwa chuoni kwa ajili ya masomo ya wiki mbili au tatu.

Baada ya hapo, amesema atajua kituo chake na anakwenda kufundishwa ubalozi ambao yeye anaona kama uvivu.

“Wakati mwingine mimi naona ubalozi kama mnafanya uvivu, maana zile itifaki ufundishwe sijui kifungo ufungeje, kidole kikaeje, sijui ukikaa juu ya meza ukaeje.

“Lakini mtu akikusema vibaya wewe usiseme vibaya mjibu politely, kitu ambacho mimi siwezi, wakinikera mimi nabwatuka tu. Nikirudi ofisini msaidizi wangu wa diplomasia ananiambia mheshimiwa lakini leo pale ulikuwa hivi, namwambia eeh… hiyo kazi yako wewe, mimi wamenikera wamesema na mimi nasema,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, amesema kazi ya wote walioapa ni kulifanya Taifa liendelee na kuitekeleza dira ya miaka 25 ijayo itakayoishia mwaka 2050.

“Sisi ndio wa kuweka msingi kama tulivyokuta msingi wengine wameweka sisi tukajenga juu, na sisi ndio wa kuweka msingi wa utekelezaji wa dira tunayokwenda kuitekeleza, kwa hiyo niombe kila mtu akatekeleze wajibu wake.”

“Mimi kwangu ni jicho, nani anacheza vipi, nikiona steps zako haziendani na ngoma ninayoipiga, basi utatupisha pembeni niangalie nani mwingine miguu yake myepesi ambaye anaweza akaendana na steps za ngoma ninayoipiga,” amesema.

Amesema katika awamu hii, hakutakuwa na mabadiliko makubwa ya viongozi, badala yake, atafanya madogo itakapotokea mmoja amestaafu au amezembea.

“Wale waliofikiri labda tukiingia kutakua na pindua meza mambo yaanze upya hapana, hii Serikali inaendelea, kwa hiyo kutakua na mabadiliko madogo, kubadilishana vituo, sekta hayo yatakuwepo, lakini mpaka mtu akithiri sana ndio atakaa pembeni asipokithiri basi tutakwenda pamoja au tutarekebishana tutakwenda pamoja,” amesema.

Amesema mabadiliko hayo aliyoyafanya yanalenga jitihada za kuongeza kasi ya utekelezaji, kuimarisha uwajibikaji, kulinganisha majukumu na vipaumbele vya Taifa letu na kuendana na kasi inayoendana na matarajio ya wananchi.

“Lengo ni kuendana na kasi ya matarajio ya wananchi. Mmeaminiwa kwa uwezo, uzoefu na uadilifu. Niwatake mkaishi na kiapo mlichoapa hapa leo, lakini pia kuna kiapo cha maadili mmesaini nakala mbili,” amesema.