Dar es Salaam. Serikali imetaka nguvu ya pamoja kati ya wadau wa sekta ya afya katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za kifafa nchini, ikiwemo maandalizi ya kuanzisha Kamati Maalum ya Kitaifa ya Wataalamu wa Mishipa ya Fahamu itakayoratibu masuala ya kifafa na magonjwa mengine ya mfumo wa fahamu.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Februari 9, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, kwa niaba ya Serikali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kifafa yaliyoandaliwa na Chama cha Kifafa Tanzania (Tea) na kufanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Dk Samizi amewahimiza wadau kuongeza juhudi za kupambana na unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na kifafa pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kuanzia ngazi ya huduma za afya ya msingi.
Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Chama cha Kifafa Tanzania na Amref Health Africa inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kukabiliana na kifafa, ingawa bado juhudi zaidi zinahitajika.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, Dk Samizi amesema ugonjwa wa kifafa bado umezungukwa na imani potofu katika jamii nyingi, hali inayosababisha wagonjwa kuchelewa kupata matibabu na kukumbana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kiuchumi.
“Katika baadhi ya jamii, kifafa bado kinaaminika kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza au unaosababishwa na uchawi. Imani hizi zimesababisha watu wanaoishi na kifafa kubaguliwa katika elimu, ajira, ndoa na maisha ya kila siku, jambo lisilokubalika,” amesema.
Akinukuu takwimu za WHO, amesema takribani watu milioni 50 duniani wanaishi na kifafa, ambapo zaidi ya asilimia 80 wanatoka katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hususan barani Afrika. Ameongeza kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni moja wanaoishi na kifafa, huku takribani watu 200,000 pekee wakipata huduma za matibabu.
Dk Samizi amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kifafa. Ameeleza kuwa upatikanaji wa dawa umeimarika, ambapo dawa ya Carbamazepine sasa inapatikana katika zaidi ya asilimia 50 ya vituo vya afya, huku Phenobarbitone ikipatikana katika zaidi ya asilimia 90.
Aidha, amesema wizara inatambua umuhimu wa sera na sheria zinazolinda haki za watu wanaoishi na kifafa, hasa katika ajira, elimu na huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Julieth Magandi, amesema hospitali hiyo imewekeza katika kuimarisha huduma za kifafa kupitia afua nne kuu, ikiwemo kuboresha huduma za watoto kwa kutumia vifaa vya kisasa na kuanzisha kitengo maalum cha uchunguzi katika Hospitali ya Mloganzila.
Naye Rais wa Tea, Profesa William Matuja, amesema elimu kwa jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya kifafa, akisisitiza kuwa jamii ikielimishwa ipasavyo wagonjwa wengi watajitokeza kupata matibabu.
Maadhimisho ya Siku ya Kifafa yaliongozwa na kaulimbiu isemayo: “Huduma za Kifafa Tanzania; Chukua Hatua Kupunguza Unyanyapaa”, ikiwa ni wito wa kuongeza uelewa na heshima kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo.