Arusha. Hivi karibuni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilizindua Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.
Imebainika kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wanaofika darasa la tatu wakiwa hawana stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu na hivyo kuathiri ubora wa elimu kwa ujumla.
Kisha ni majuzi tena tumepata ripoti kwamba nusu ya watahiniwa kidato cha nne waliambulia daraja la nne na sifuri.
Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 2 Februari, 2026, tumesona ripoti isemayo kwamba asilimia 53.74 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2025 walipata daraja la nne na sifuri. Hiyo ni zaidi ya nusu ya watahiniwa wote wa mitihani hiyo.
Hili pia ni tatizo. Ijapokuwa iliripotiwa kwamba matokeo ya kidato cha nne mwaka 2025 ni bora kuliko yale ya mwaka 2024, bado naona tuna shida kubwa katika elimu yetu kama Taifa.
Hebu fikiria idadi kubwa ya watoto wa darasa la tatu hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Halafu asilimia 53.74 ya wanafunzi wa kidato cha nne wanapata daraja la tatu na sifuri. Haya ni matatizo makubwa katika elimu yetu.
Mikakati halisi au siasa?
Kama taifa hatuna uhaba wa uzinduzi wa mikakati ya elimu mara kwa mara, lakini bado tunaona changamoto zilizotajwa hapo juu. Ni kama tunafanya hivyo kisiasa tu kuonyesha ulimwengu kwamba tuna mipango na mikakati mingi ya kuboresha elimu, lakini mwishowe inakuwa kama ni nguvu ya soda.
Wadau wa elimu wamesema mara nyingi kwamba badala ya kuzindua mikakati kila mara, tutekeleze kwanza mipango tuliyokwisha kujiwekea kama vile kuwa na walimu wa kutosho shuleni, madawati ya kutosha, vitabu, maktaba na maabara za kutosha. Pia imesemwa mara nyingi kwamba masilahi ya walimu yaboreshwe na idara ya elimu ipata bajeti ya kutosha.
Naunga mkono mawazo hayo, lakini kwa leo napenda kujikita katika ukweli mmoja ambao mataifa yote yenye elimu bora wanatambua na kutekeleza nao ni huu: bila ufundishaji bora hakuna ujifunzaji bora. Kwa maneno mengine, elimu bora inategemea walimu bora.
Mwalimu ndio kila kitu
Serikali, wizara husika, wadau na sisi wote wananchi tunaweza kutayarisha miundombino yote inayotakiwa kama vile, mitalaa, madarasa, madawati, vitabu, maabara na vifaa vingine vyote vinavyotakiwa, lakini tusipomtayarisha mwalimu bora hatutafikia malengo tunayoyatamani.
Hapa mwalimu ni kila kitu. Shule ni mwalimu. Elimu ni mwalimu. Yeye ndiye atatekeleza yale yote tunayoyapanga katika wizara ya elimu.
Yeye ndiye anawakilisha taifa darasani. Yeye ndiye anawakilisha familia darasani. Yeye ndiye mwakilishi wetu darasani na hata nje ya darasa, katika uadilifu, utu, ubunifu, uzalendo, haki, amani na utulivu wa taifa.
Yeye ndiye anayekaa na mtoto wetu saa nyingi kuliko wazazi asubuhi hadi jioni, na yeye ndiye yuko na mtoto wetu kwa muda mwingi zaidi kuanzia Januari hadi Desemba.
Unaweza kusema kwamba huyu mwalimu tumemtwisha msalaba mzito sana na kazi yake ni takatifu.
Nikifikiria kwa kina kazi ya mwalimu naanza hata kuiogopa hii kazi, ni kama inaogopesha kuwa mwalimu kwa sababu ni wajibu mzito sana, na mtu yeyote anayetambua uzito wake hatausogelea kijuujuu.
Hebu fikiria msomaji, wewe ni mwalimu darasani, una watoto 40 wadogo shule ya awali au darasa la kwanza, wanakutegemea wewe, wazazi wao wanakutegemea wewe, jamii inakuangalia wewe, serikali inakukazia macho, dunia inakupiga darubini, hebu tafakari hayo yote. Inaogopesha. Kama haikuogopeshi hustahili kuwa mwalimu.
Nakumbuka nikiwa mtoto shule ya awali na msingi kuna watu aina tatu walioheshimika sana katika jamii yetu: viongozi wa dini, viongozi wa serikali na walimu.
Ulikuwepo msemo: huyu ana mke mmoja kama mwalimu. Hii ilikuwa na maana kwamba huyu mtu ni mwaminifu katika ndoa yake kama mwalimu alivyo mwadilifu katika jamii.
Heshima tuliyowapa walimu wetu ilikuwa sawa na ile tuliyowapa viongozi wa dini.
Mwalimu bora atamsogelea mwanafunzi kwa tahadhari kubwa, akijua Mungu yupo ndani ya huyo mwanafunzi akimwongoza, na hivyo mwalimu asikufuru nafasi hiyo, asimdhalilishe Mungu aliyemuumba huyo mtoto na anayemwongoza huyo mtoto.
Ni mtu mzembe wa kutisha atakayethubutu kuingia katika uwanja alipo Mungu bila tafadhari kubwa na uangalifu uliotukuka.
Huenda msomaji ukafikiri kwamba haya ninayoyasema ni kama ndoto za Abunuwasi, ni kama ninatamani mwalimu awe na uwezo ambao kibinadamu hauwezekani.
Hii si kweli. Iliwezekana nikiwa mtoto, kwa nini isiwezekane sasa, hata kama dunia imebadilika? Ninawafahamu sasa hivi walimu walio na sifa hizi nilizotaja hapa, ijapokuwa si wengi. Inawezekana. Tujipange kwa kutambua hili: penye nia pana njia.
Tufanyeje?
Sasa tufanyeje? Napendekeza tuweke nguvu kubwa katika kutayarisha walimu tunaowataka ili malengo yetu ya kuboresha elimu yatimie.
Tuboreshe masilahi ya walimu waliopo ili wajenge tabia ya kupenda kazi yao. Tumpe heshima mwalimu ili jamii ipende kumheshimu mwalimu, na wanafunzi wetu wawaheshimu walimu wao.
Mwalimu anayependwa na kuheshimiwa na wanafunzi wake na jamii yake anawafanya wanafunzi watamani kuwa walimu.
Anawafanya wapende shule. Mimi ni mwalimu na profesa kwa vile nilitamani kufuate nyayo za walimu walionifundisha.
Pili, kama taifa na kama wizara ya elimu, tukae chini tupange namna ya kuwaheshimu walimu waliopo na kuwapa masilahi stahiki. Mishahara yao iboreshwe, na bajeti yetu ya elimu iwape kipaumbele.
Tatu, tujipange upya katika kuchagua wanafunzi watakaoingia vyuo vya ualimu. Rasimu yetu ijikite sana katika jambo hili.
Sehemu kubwa ya mipango yetu ya kuboresha elimu iweke kipaumbele katika kuchagua walimu watarajiwa na namna ya kuwatayarisha. Tukumbuke: shule ni mwalimu, elimu ni mwalimu.
Nne, tuangalie uzoefu wa mataifa yanayofanya vizuri katika elimu kama vile Finland, Japan, Korea ya Kusini na kadhalika, kisha tupendekeze mpango mpya wa kuchagua na kutayarisha walimu bora. Wapo walimu wengi wastaafu wenye umri mkubwa. Tuchukue mawazo yao na mapendekezo yao. Tutambue ukweli huu: ufundishaji bora huzaa ujifunzaji bora.
Prof. Raymond S. Mosha
(255) 769 417 886; [email protected]