Arusha. Thamani ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini imeongezeka kutoka Sh10.43 trilioni Juni 2020 hadi kufikia Sh24.20 trilioni Desemba 2025.
Aidha, Serikali imezindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na skimu ya wananchi waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi, ambayo hadi Desemba 2025 tayari wanachama 509,000 kutoka makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, mamalishe, bodaboda na bajaji wamejiandikisha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi huo, amesema maboresho katika sekta ya kinga ya jamii yamewezesha kulipa malimbikizo ya madeni ya Sh4.26 trilioni, yanayohusiana na michango ya wanachama wa Mfuko wa PSSF (Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma) kabla ya Juni 1999.
Waziri Sangu amefafanua kuwa katika kipindi cha Juni 2020 hadi Desemba 2025, thamani ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliongezeka kutoka Sh4.36 trilioni, huku PSSSF ukiongezeka kutoka Sh5.74 trilioni hadi Sh12.96 trilioni. Pia, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) uliongezeka kutoka Sh333.46 bilioni hadi Sh844.41 bilioni.
Michango ya wanachama pia imeongeza thamani ya mifuko. NSSF iliongezeka kutoka Sh1.067 bilioni hadi Sh1.246 bilioni, huku PSSF ikiongezeka kutoka Sh1.272 bilioni hadi Sh1.346 bilioni. Uwekezaji wa mifuko hiyo umefanyika katika hati fungani za Serikali na kampuni binafsi, miliki ardhi, hisa katika masoko ya mitaji, amana za benki na uwekezaji wa pamoja.
“Pamoja na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya kinga ya jamii, ninamshukuru Rais kwa azma yake ya kulitambua deni la Sh4.46 trilioni la michango ya wanachama wa PSSSF kabla ya Juni 1999. Kiasi kilicholipwa ni Sh4.26 trilioni sawa na asilimia 95 ya deni lote. Serikali inaendelea na uhakiki wa kiasi cha deni kilichobaki,” amesema Sangu.
Amesema sera hiyo inalenga kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa masuala ya kinga ya jamii, sambamba na utekelezaji wa Dira 2050 na shabaha yake ya kupata huduma jumuishi za hifadhi ya jamii kwa wote. Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria ili wananchi wafanye kazi na kupata kinga dhidi ya majanga kama uzee, maradhi, ulemavu na ukosefu wa kipato.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kusimamia mifuko hiyo kwa karibu, huku viongozi wa bodi na menejimenti wakihakikisha kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika uwekezaji wa fedha za wanachama, pamoja na kuhakikisha utoaji wa huduma bora na taarifa sahihi kwa wanachama.
Skimu ya wananchi waliojiajiri inalenga kufikia wananchi zaidi ya milioni 5.5 ifikapo Juni 2031. Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mary Maganga, amesema sera hiyo iliandaliwa kuanzia 2023 kwa ushauri wa wadau wa kimataifa kama Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef), Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Chakoma, amesisitiza kuwa kamati hiyo haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa sera hiyo muhimu katika kuimarisha sekta ya kinga ya jamii.